Agano la Kale

Agano Jipya

2 Samueli 23:15-30 Biblia Habari Njema (BHN)

15. Daudi akasema kwa hamu kubwa, “Laiti mtu angeweza kunipa maji ya kunywa kutoka katika kisima cha Bethlehemu, kilicho karibu na lango la mji!”

16. Wale mashujaa wake watatu walitoka, wakapenya katikati ya kambi ya jeshi la Wafilisti, wakaenda na kuchota maji katika kisima cha Bethlehemu, karibu na lango la mji, wakamletea Daudi. Lakini Daudi alikataa kuyanywa, na badala yake, akayamwaga chini kama tambiko kwa Mwenyezi-Mungu,

17. akisema, “Kamwe, sina haki ya kunywa maji haya, ee Mwenyezi-Mungu; je, haya si kama damu ya wale walioyahatarisha maisha yao kuyaleta maji haya?” Kwa hiyo, Daudi hakuyanywa maji hayo. Hayo ndiyo mambo waliyotenda wale mashujaa watatu.

18. Abishai nduguye Yoabu, mwana wa Seruya, alikuwa mkuu wa mashujaa thelathini. Yeye alipigana kwa mkuki wake dhidi ya watu 300, akawaua, akajipatia jina miongoni mwa wale mashujaa watatu.

19. Je, huyo hakuwa mashuhuri zaidi miongoni mwa mashujaa watatu? Kwa hiyo akawa kamanda wao, lakini hakuwa shujaa kama wale mashujaa watatu.

20. Naye Benaya mwana wa Yehoyada, kutoka Kabzeeli, alikuwa askari shujaa ambaye alifanya mambo mengi ya ajabu. Aliwaua mashujaa wawili kutoka Moabu, na siku moja wakati wa theluji, alishuka shimoni na kuua simba.

21. Vilevile, aliliua jitu la Misri. Mmisri huyo alikuwa na mkuki, lakini Benaya alimwendea akiwa na fimbo tu, akamnyanganya mkuki huo, na kumwua Mmisri huyo kwa mkuki wake mwenyewe.

22. Benaya, mwana wa Yehoyada alifanya mambo haya, akajipatia jina miongoni mwa wale mashujaa watatu.

23. Basi, akawa mashuhuri kati ya wale mashujaa thelathini, ingawa hakuwa kama wale mashujaa watatu. Na Daudi akampa cheo cha mkuu wa walinzi wake binafsi.

24. Asaheli, nduguye Yoabu, alikuwa mmoja wa mashujaa thelathini. Mashujaa wengine wa Daudi walikuwa: Elhanani, mwana wa Dodo wa Bethlehemu;

25. Shama, Mharodi; Elika, Mharodi;

26. Helesi, Mpalti; Ira, mwana wa Ikeshi, Mtekoa;

27. Abiezeri, Mwanathothi; Mebunai, Mhushathi;

28. Salmoni, Mwahohi; Maharai, Mnetofathi;

29. Helebu mwana wa Baana, Mnetofathi; Itai mwana wa Ribai, toka Gibea katika Benyamini;

30. Benaya, Mpirathoni; Hidai, wa vijito vya Gaashi;

Kusoma sura kamili 2 Samueli 23