Agano la Kale

Agano Jipya

2 Samueli 23:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Yafuatayo ni maneno ya mwisho ya Daudi. Ni ujumbe wa Daudi mwana wa Yese; ujumbe wa mtu ambaye Mungu alimfanya awe mkuu. Mungu wa Yakobo alimteua Daudi kuwa mfalme na maneno yake Waisraeli walifurahi kuyaimba.

2. “Roho ya Mwenyezi-Mungu imesema kwa njia yangu,aliyaweka maneno yake kinywani mwangu.

3. Mungu wa Israeli amesema,Mwamba wa Israeli ameniambia,‘Mtu anapowatawala watu kwa haki,atawalaye kwa kumcha Mungu,

4. yeye ni kama mwanga wa asubuhi,jua linapochomoza asubuhi isiyo na mawingu;naam, kama mvua inayootesha majani ardhini’.

5. Hivyo ndivyo Mungu alivyoujalia ukoo wangu.Maana amefanya nami agano la kudumu milele;agano kamili na thabiti.Naye atanifanikisha katika matakwa yangu yote.

6. Lakini wasiomcha Munguwote ni kama miiba inayotupwa tu,maana haiwezi kuchukuliwa kwa mkono;

7. kuishika, lazima kutumia chuma au mpini wa mkuki.Watu hao wataangamizwa kabisa kwa moto.”

8. Yafuatayo ni majina ya mashujaa aliokuwa nao Daudi: Yosheb-bashebethi, Mtakmoni, aliyekuwa kiongozi wa wale watatu, yeye alipigana kwa mkuki wake, akaua watu 800 wakati mmoja.

9. Halafu aliyefuata miongoni mwa wale mashujaa watatu alikuwa Eleazari mwana wa Dodo, wa ukoo wa Mwahohi. Siku moja, Eleazari alikuwa pamoja na Daudi walipowatukana Wafilisti waliokuwa wamekusanyika kupigana vita. Waisraeli waliwakimbia Wafilisti.

10. Lakini Eleazari alisimama imara na kupigana na Wafilisti mpaka mkono wake uliposhindwa kupinda, ukabaki umeshikilia upanga wake. Siku hiyo, Mwenyezi-Mungu alijipatia ushindi mkubwa. Baada ya ushindi huo, Waisraeli walirudi mahali alipokuwa Eleazari na kujipatia nyara za bure kutoka kwa Wafilisti waliouawa.

11. Shujaa wa tatu alikuwa Shama mwana wa Agee, Mharari. Wafilisti walikusanyika huko Lehi, mahali palipokuwa na shamba la dengu nyingi, nao Waisraeli waliwakimbia Wafilisti.

Kusoma sura kamili 2 Samueli 23