Agano la Kale

Agano Jipya

2 Samueli 2:23-32 Biblia Habari Njema (BHN)

23. Lakini Asaheli alikataa. Hivyo Abneri akampiga mkuki tumboni kinyumenyume, na mkuki huo ukatokeza mgongoni kwa Asaheli. Asaheli akaanguka chini, na kufa papo hapo. Watu wote waliofika mahali alipofia Asaheli, walisimama kimya.

24. Lakini Yoabu na Abishai walimfuatia Abneri. Jua lilipokuwa linatua, wakafika kwenye mlima wa Ama, ulioko mashariki ya Gia, katika barabara iendayo jangwa la Gibeoni.

25. Watu wa kabila la Benyamini wakajikusanya pamoja wakawa nyuma ya Abneri, hivyo wakaunda kikosi chao; nao wakasimama juu ya mlima.

26. Kisha Abneri akamwita Yoabu, “Je, tutapigana siku zote? Je, huoni kwamba mwisho utakuwa mchungu? Je, utaendelea kwa muda gani bila kuwashawishi watu wako waache kuwaandama ndugu zao?”

27. Yoabu akamwambia, “Naapa kwa Mungu aliye hai, kwamba kama hungesema jambo hilo, hakika watu wangu wangeendelea kuwaandama ndugu zao hadi kesho asubuhi.”

28. Hivyo, Yoabu akapiga tarumbeta na watu wakaacha kuwafuatia watu wa Israeli, wala hawakupigana zaidi.

29. Abneri na watu wake walipita bonde la Araba usiku kucha. Wakavuka mto Yordani, wakatembea mchana kutwa hadi Mahanaimu.

30. Yoabu aliporudi kutoka kumfuatia Abneri, aliwakusanya watu wake wote, akagundua kuwa watumishi kumi na tisa wa Daudi walikosekana, licha ya Asaheli.

31. Lakini watumishi wa Daudi walikuwa wamewaua watu 360 kutoka kabila la Benyamini pamoja na watu wa Abneri.

32. Yoabu na watu wake waliuchukua mwili wa Asaheli, wakauzika kwenye kaburi la baba yake, lililoko huko Bethlehemu. Yoabu na watu wake walitembea usiku kucha, na kulipokucha wakafika mjini Hebroni.

Kusoma sura kamili 2 Samueli 2