Agano la Kale

Agano Jipya

2 Samueli 2:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Baada ya mambo haya, Daudi alimwomba Mwenyezi-Mungu shauri, akasema, “Je, niende kwenye mji mmojawapo wa miji ya Yuda?” Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Nenda!” Daudi akamwuliza, “Niende mji upi?” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Nenda kwenye mji wa Hebroni.”

2. Hivyo, Daudi alikwenda Hebroni, pamoja na wake zake wawili, Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili, mjane wa Nabali, kutoka mji wa Karmeli.

3. Aliwachukua watu wake, kila mtu akiwa pamoja na jamaa yake; nao wakafanya makao yao katika miji iliyokuwa kandokando ya Hebroni.

4. Watu wa Yuda walimwendea Daudi huko Hebroni wakampaka mafuta awe mfalme wao.Daudi aliposikia kuwa watu wa Yabesh-gileadi ndio waliomzika Shauli,

5. aliwatuma watu huko Yabesh-gileadi na ujumbe: “Mwenyezi-Mungu na awabariki kwa maana mlionesha utii wenu kwa Shauli, bwana wenu, kwa kumzika.

6. Sasa, Mwenyezi-Mungu awafadhili na kuwa mwaminifu kwenu. Nami nitawatendea mema kutokana na jambo mlilolitenda.

7. Lakini muwe imara na mashujaa. Shauli, bwana wenu, amekufa, na watu wa Yuda wamenipaka mafuta niwe mfalme wao.”

8. Abneri mwana wa Neri, kamanda wa jeshi la Shauli alikuwa amemchukua Ishboshethi mwana wa Shauli na kumpeleka huko Mahanaimu.

9. Huko, Abneri akamtawaza Ishboshethi kuwa mfalme wa nchi ya Gileadi, Ashuru, Yezreeli, Efraimu na Benyamini na Israeli yote.

10. Ishboshethi alikuwa na umri wa miaka arubaini alipoanza kuitawala Israeli, naye alitawala kwa muda wa miaka miwili. Lakini kabila la Yuda lilimfuata Daudi.

11. Daudi alikuwa mfalme wa kabila la Yuda kwa muda wa miaka saba na nusu, makao yake yalikuwa huko Hebroni.

12. Abneri mwana wa Neri, pamoja na maofisa wa Ishboshethi, mwana wa Shauli, waliondoka Mahanaimu na kwenda Gibeoni.

13. Yoabu mwana wa Seruya na watumishi wengine wa Daudi, nao walitoka na kukutana na Abneri na watu aliokuwa nao kwenye bwawa lililoko huko Gibeoni. Kikosi kimoja upande mmoja wa bwawa na kingine upande mwingine.

Kusoma sura kamili 2 Samueli 2