Agano la Kale

Agano Jipya

2 Samueli 17:5-15 Biblia Habari Njema (BHN)

5. Kisha, Absalomu akasema, “Mwiteni Hushai pia, yule mtu wa Arki, tusikie analotaka kusema.”

6. Hushai alipofika kwa Absalomu, Absalomu alimwuliza, “Hivyo ndivyo alivyosema Ahithofeli. Je, tufanye kama alivyotushauri? Kama sivyo, basi, tuambie lako.”

7. Hushai akamwambia Absalomu, “Wakati huu, shauri alilolitoa Ahithofeli si jema.”

8. Zaidi ya hayo, Hushai akamwambia, “Wewe unajua kwamba baba yako na watu wake ni mashujaa na kwamba wamekasirishwa kama dubu jike nyikani aliyenyanganywa watoto wake. Mbali na hayo, unajua kwamba baba yako ni bingwa wa vita. Yeye hatakaa usiku kucha pamoja na watu wake.

9. Hata sasa amekwisha jificha kwenye mojawapo ya mapango yaliyoko huko au mahali pengine. Mtu yeyote atakayesikia kuuawa kwa watu katika mashambulizi ya kwanza atasema kuwa mauaji yametokea katika kundi la wafuasi wa Absalomu.

10. Watu wako watakaposikia hivyo, hata wale watu wako walio shupavu, wenye mioyo shupavu kama ya simba, watavunjika moyo kabisa kwa hofu. Maana, Waisraeli wote wanajua kuwa baba yako ni shujaa na wote walio pamoja naye ni watu hodari.

11. Shauri langu ni kwamba, uwakusanye kwako watu wote wa Israeli tangu Dani hadi Beer-sheba, upande wa kusini, wawe wengi kama mchanga wa bahari, na wewe mwenyewe binafsi uende vitani.

12. Nasi tutamwendea Daudi mahali popote anapoweza kupatikana na tutamvamia kama umande unavyoiangukia ardhi. Basi, hakuna atakayesalia hata kama atakuwa yeye mwenyewe au watu wake wote walio pamoja naye.

13. Iwapo atakimbilia mji fulani, basi, watu wote wa Israeli wataleta kamba na kuuburuta mji huo, hadi bondeni, kisibaki chochote hata jiwe dogo la mji huo.”

14. Absalomu pamoja na watu wote wa Israeli wakasema, “Shauri la Hushai ni bora kuliko shauri la Ahithofeli.” Wakakataa shauri la Ahithofeli kwa kuwa Mwenyezi-Mungu alikuwa amepanga kulishinda shauri jema la Ahithofeli ili aweze kumletea Absalomu maafa.

15. Kisha Hushai akawaambia makuhani Sadoki na Abiathari jinsi Ahithofeli na yeye mwenyewe walivyomshauri Absalomu na wazee wa Israeli.

Kusoma sura kamili 2 Samueli 17