Agano la Kale

Agano Jipya

2 Samueli 17:19-29 Biblia Habari Njema (BHN)

19. Mwanamke mwenye nyumba hiyo akachukua kifuniko na kukifunika kisima hicho, halafu akaanika nafaka juu ya kifuniko. Habari hizo hazikujulikana.

20. Watumishi wa Absalomu walipowasili kwa huyo mwanamke, wakamwambia, “Wako wapi Ahimaasi na Yonathani?” Yule mwanamke akawaambia, “Wamekwenda ngambo ya kijito.” Walipowatafuta na kuwakosa, wakarudi mjini Yerusalemu.

21. Baada ya watumishi wa Absalomu kuondoka, Yonathani na Ahimaasi walitoka kisimani, wakaenda kwa mfalme Daudi na kumpasha habari. Wakamwambia, “Ondoka, uende ngambo ya mto, kwa sababu Ahithofeli amemshauri Absalomu dhidi yako.”

22. Kwa hiyo, Daudi akaondoka na watu wote waliokuwa pamoja naye, wakavuka mto Yordani. Ilipofika asubuhi hakuna mtu aliyebaki nyuma bila kuvuka mto Yordani.

23. Ahithofeli alipoona kwamba shauri lake halikufuatwa, alitandika punda wake, akaenda nyumbani, kwenye mji wake. Alipofika huko, alipanga vizuri mambo ya nyumbani kwake, akajinyonga. Akafariki na kuzikwa kwenye kaburi la baba yake.

24. Basi, Daudi akaenda Mahanaimu. Absalomu akavuka mto Yordani na watu wote wa Israeli.

25. Wakati huo, Absalomu alikuwa amemweka Amasa kuwa mkuu wa jeshi badala ya Yoabu. Amasa alikuwa mwana wa Yithra, Mwishmaeli. Mama yake aliitwa Abigali binti wa Nahashi, aliyekuwa dada yake, Seruya, mama yake Yoabu.

26. Absalomu pamoja na watu wa Israeli walipiga kambi yao katika nchi ya Gileadi.

27. Daudi alipowasili Mahanaimu, Shobi mwana wa Nahashi Mwamoni, kutoka mji wa Raba; Makiri mwana wa Amieli kutoka mji wa Lo-debari, pamoja na Barzilai Mgileadi kutoka mji wa Rogelimu,

28. walipeleka vitanda, mabirika, vyombo vya udongo, ngano, shayiri, unga, bisi, kunde na dengu,

29. asali, siagi, kondoo na jibini kutoka mifugo yao kwa ajili ya Daudi pamoja na watu aliokuwa nao. Maana walisema, “Watu hawa wana njaa, wamechoka na wana kiu kwa ajili ya kusafiri jangwani.”

Kusoma sura kamili 2 Samueli 17