Agano la Kale

Agano Jipya

2 Samueli 15:5-16 Biblia Habari Njema (BHN)

5. Zaidi ya hayo, Absalomu alinyosha mkono wake akamkumbatia na kumbusu mtu yeyote aliyekuja kumwinamia na kumsujudu.

6. Basi, hivyo ndivyo Absalomu alivyowatendea Waisraeli wote waliokuja kutafuta uamuzi wa mfalme. Kwa kufanya hivyo, Absalomu aliiteka mioyo ya Waisraeli.

7. Baada ya miaka minne, Absalomu alimwambia mfalme, “Tafadhali uniruhusu niende huko Hebroni ili kutimiza nadhiri yangu ambayo nilimwekea Mwenyezi-Mungu;

8. maana, mimi mtumishi wako, nilipoishi kule Geshuri katika Aramu, nilimwekea Mwenyezi-Mungu nadhiri nikisema kuwa kama Mwenyezi-Mungu atanirudisha mjini Yerusalemu basi, nitamwabudu yeye.”

9. Mfalme akamwambia, “Basi, nenda kwa amani.” Absalomu akaondoka kwenda Hebroni.

10. Lakini Absalomu alituma wajumbe kwa siri katika makabila yote ya Israeli, wakasema, “Mara moja mtakaposikia mlio wa tarumbeta, semeni, ‘Absalomu ni mfalme katika Hebroni!’”

11. Absalomu alipokwenda huko Hebroni, alikwenda na watu 200 aliowaalika kutoka Yerusalemu, nao walikwenda huko kwa nia njema, wala hawakujua chochote kuhusu mpango wa Absalomu.

12. Wakati Absalomu alipokuwa akitoa tambiko, alituma ujumbe mjini Gilo kumwita Ahithofeli, Mgilo, aliyekuwa mshauri wa mfalme Daudi. Uasi wa Absalomu ukazidi kupata nguvu na watu walioandamana naye wakazidi kuongezeka.

13. Mjumbe fulani alipomwendea Daudi na kumwambia, “Watu wa Israeli wamevutwa na Absalomu!”

14. Basi, Daudi akawaambia watumishi wake waliokuwa naye mjini Yerusalemu, “Inukeni tukimbie, la sivyo, hatutaweza kumwepa Absalomu. Tufanye haraka kuondoka asije akatuletea maafa na kuuangamiza mji kwa mapanga.”

15. Lakini watumishi wake wakamwambia, “Sisi watumishi wako, bwana wetu mfalme, tuko tayari kufanya lolote unaloamua.”

16. Basi, mfalme akaondoka pamoja na jamaa yake, lakini akawaacha masuria wake kumi wakishughulika na kazi za nyumbani.

Kusoma sura kamili 2 Samueli 15