Agano la Kale

Agano Jipya

2 Samueli 15:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Baada ya tukio hilo, Absalomu alijipatia gari, farasi na watu hamsini wa kumtangulia.

2. Absalomu alizoea kuamka asubuhi na mapema na kwenda kusimama kwenye njia inayoelekea kwenye lango la mji. Mtu yeyote aliyekuwa na madai ambayo alitaka kuyapeleka kwa mfalme ili kupata uamuzi wake, Absalomu humwita mtu huyo kando na kumwuliza, “Unatoka mji gani?” Kama mtu huyo akisema ametoka mji fulani wa kabila la Israeli,

3. Absalomu humwambia, “Madai yako ni ya haki kabisa. Lakini hakuna mtu yeyote aliyeteuliwa na mfalme kukusikiliza.”

4. Tena, Absalomu humwambia, “Laiti mimi ningekuwa mwamuzi wa Israeli! Kila mtu mwenye madai au shauri angekuja kwangu, nami ningempa haki yake!”

5. Zaidi ya hayo, Absalomu alinyosha mkono wake akamkumbatia na kumbusu mtu yeyote aliyekuja kumwinamia na kumsujudu.

6. Basi, hivyo ndivyo Absalomu alivyowatendea Waisraeli wote waliokuja kutafuta uamuzi wa mfalme. Kwa kufanya hivyo, Absalomu aliiteka mioyo ya Waisraeli.

7. Baada ya miaka minne, Absalomu alimwambia mfalme, “Tafadhali uniruhusu niende huko Hebroni ili kutimiza nadhiri yangu ambayo nilimwekea Mwenyezi-Mungu;

8. maana, mimi mtumishi wako, nilipoishi kule Geshuri katika Aramu, nilimwekea Mwenyezi-Mungu nadhiri nikisema kuwa kama Mwenyezi-Mungu atanirudisha mjini Yerusalemu basi, nitamwabudu yeye.”

9. Mfalme akamwambia, “Basi, nenda kwa amani.” Absalomu akaondoka kwenda Hebroni.

10. Lakini Absalomu alituma wajumbe kwa siri katika makabila yote ya Israeli, wakasema, “Mara moja mtakaposikia mlio wa tarumbeta, semeni, ‘Absalomu ni mfalme katika Hebroni!’”

11. Absalomu alipokwenda huko Hebroni, alikwenda na watu 200 aliowaalika kutoka Yerusalemu, nao walikwenda huko kwa nia njema, wala hawakujua chochote kuhusu mpango wa Absalomu.

12. Wakati Absalomu alipokuwa akitoa tambiko, alituma ujumbe mjini Gilo kumwita Ahithofeli, Mgilo, aliyekuwa mshauri wa mfalme Daudi. Uasi wa Absalomu ukazidi kupata nguvu na watu walioandamana naye wakazidi kuongezeka.

13. Mjumbe fulani alipomwendea Daudi na kumwambia, “Watu wa Israeli wamevutwa na Absalomu!”

14. Basi, Daudi akawaambia watumishi wake waliokuwa naye mjini Yerusalemu, “Inukeni tukimbie, la sivyo, hatutaweza kumwepa Absalomu. Tufanye haraka kuondoka asije akatuletea maafa na kuuangamiza mji kwa mapanga.”

Kusoma sura kamili 2 Samueli 15