Agano la Kale

Agano Jipya

2 Samueli 14:4-14 Biblia Habari Njema (BHN)

4. Huyo mwanamke kutoka Tekoa akaenda kwa mfalme, akaanguka kifudifudi, mbele ya mfalme, akasujudu, akamwambia, “Ee mfalme, nisaidie.”

5. Mfalme akamwambia, “Una shida gani?” Yule mwanamke akajibu, “Nasikitika, mimi ni mjane, mume wangu amekufa.

6. Nilikuwa na watoto wa kiume wawili. Siku moja, walipokuwa mbugani, walianza kugombana. Kwa vile hapakuwa na mtu yeyote wa kuwaamua, mmoja akampiga mwenzake, akamuua.

7. Sasa ndugu zangu wote wamenigeuka mimi mtumishi wako; wanataka nimtoe kwao mtoto aliyemuua mwenzake ili wamuue kwa kuyaangamiza maisha ya ndugu yake. Hivyo, watamuua huyu ambaye sasa ndiye mrithi. Wakifanya hivyo, watazima kabisa tumaini langu lililobakia, na mume wangu hataachiwa jina wala mzawa duniani.”

8. Mfalme akamwambia yule mwanamke, “Rudi nyumbani nitaamuru jambo lako liangaliwe.”

9. Yule mwanamke kutoka Tekoa akasema, “Bwana wangu mfalme, hatia yote na iwe juu yangu na juu ya jamaa ya baba yangu. Hivyo, wewe na ufalme wako msiwe na hatia.”

10. Mfalme akamwambia, “Mtu yeyote akikutishia mlete kwangu na hatakuja kukugusa tena.”

11. Yule mwanamke akamwambia, “Tafadhali, mfalme, niombee kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ili yule ndugu yangu ambaye angelipiza kisasi cha mauaji ya mwanangu asifanye hatia nyingine kubwa ya kumwua yule mtoto wangu mwingine.” Mfalme Daudi akamwambia, “Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo, hakuna hata unywele mmoja wa mwanao utakaoanguka chini.”

12. Yule mwanamke akamwambia, “Nakuomba, mimi mtumishi wako, uniruhusu niseme neno moja kwako mfalme.” Mfalme akamwambia, “Sema”.

13. Yule mwanamke akamwambia, “Kwa nini basi, umepanga uovu huu dhidi ya watu wa Mungu? Kulingana na uamuzi wako juu ya jambo hilo wewe mwenyewe umejihukumu kuwa na hatia kwa sababu humruhusu mwanao arudi nyumbani kutoka alikokimbilia.

14. Sisi sote lazima tutakufa. Sisi ni kama maji yaliyomwagika chini ambayo hayazoleki. Hata Mungu hafanyi tofauti kwa mtu huyu na tofauti kwa mwingine; yeye hutafuta njia ili waliopigwa marufuku, wakakimbia, wapate kurudi.

Kusoma sura kamili 2 Samueli 14