Agano la Kale

Agano Jipya

2 Samueli 13:1-15 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Absalomu, alikuwa na dada yake mzuri aliyeitwa Tamari. Muda si muda, Amnoni, mtoto mwingine wa kiume wa Daudi, akampenda sana Tamari.

2. Amnoni aliteseka sana hata akajifanya mgonjwa kwa sababu ya dada yake Tamari hasa kwa vile Tamari alikuwa bikira, na ilionekana jambo lisilowezekana kwa Amnoni kufanya chochote naye.

3. Lakini Amnoni alikuwa na rafiki aliyeitwa Yonadabu, mtoto wa Shama, ndugu ya Daudi. Yonadabu alikuwa mtu mwerevu sana.

4. Yonadabu akamwambia Amnoni, “Wewe ni mtoto wa mfalme, kwa nini unakonda na unaonekana huna furaha kila siku? Mbona hutaki kuniambia.” Amnoni akamwambia, “Nampenda Tamari, dada ya ndugu yangu Absalomu.”

5. Yonadabu akamwambia, “Wewe jilaze kitandani ukidai kuwa u mgonjwa. Baba yako atakapokuja kukuona, wewe msihi ukisema, ‘Mruhusu dada yangu, Tamari, aje aniletee mkate nipate kula na aniandalie chakula mbele yangu ili nikione naye mwenyewe anilishe.’”

6. Hivyo, Amnoni akaendelea kulala kitandani, akijifanya mgonjwa. Mfalme alipokwenda kumwona, Amnoni alimwambia, “Nakuomba, Tamari aje hapa anitengenezee mikate michache huku nikimwangalia. Halafu yeye mwenyewe anilishe.”

7. Hivyo, Daudi alipeleka ujumbe kwa Tamari kwamba aende nyumbani kwa kaka yake Amnoni, akamtengenezee chakula.

8. Tamari alikwenda huko, akamkuta Amnoni amelala. Akachukua unga, akaukanda, na kuoka mikate mbele ya Amnoni.

9. Mikate hiyo ilipokuwa tayari, Tamari akaiopoa kutoka kikaangoni. Akampelekea Amnoni, lakini Amnoni alikataa kula, akasema kila mmoja na atolewe nje, na wote wakaondoka.

10. Kisha, Amnoni akamwambia Tamari, “Sasa niletee mikate hiyo chumbani kwangu, halafu unilishe.” Tamari aliichukua mikate aliyoiandaa na kuipeleka chumbani kwa kaka yake Amnoni.

11. Hapo, alipokuwa anampatia mikate hiyo, Amnoni alimkamata na kumwambia, “Njoo ulale nami.”

12. Tamari akamwambia, “Sivyo, kaka yangu, usinilazimishe. Kitendo hiki hakifanyiki katika Israeli. Usifanye kitendo hiki cha kipumbavu.

13. Kwa upande wangu, siwezi kuvumilia aibu hiyo. Na kwa upande wako, utakuwa mmoja wa wapumbavu wa Israeli. Basi, mimi nakusihi uzungumze na mfalme kwani hatakukataza kunioa.”

14. Lakini Amnoni hakutaka kumsikiliza na kwa kuwa alimzidi nguvu, alimlazimisha, akalala naye.

15. Kisha, Amnoni akamchukia Tamari kupita kiasi. Akamchukia Tamari kuliko alivyompenda hapo awali. Akamwambia Tamari, “Ondoka mara moja.”

Kusoma sura kamili 2 Samueli 13