Agano la Kale

Agano Jipya

2 Samueli 11:8-22 Biblia Habari Njema (BHN)

8. Halafu Daudi alimwambia Uria, “Rudi nyumbani kwako ukanawe miguu yako.” Uria alitoka nyumbani kwa mfalme, na mara mfalme akampelekea zawadi.

9. Lakini Uria hakurudi nyumbani kwake, bali alilala pamoja na watumishi wote wa bwana wake kwenye lango la ikulu.

10. Daudi alipoambiwa kwamba Uria hakwenda nyumbani kwake, Daudi alimwuliza Uria, “Wewe umetoka safari, kwa nini hukuenda nyumbani kwako?”

11. Uria alimjibu Daudi “Sanduku la agano, pamoja na majeshi yote ya Israeli na Yuda yanakaa kwenye vibanda vitani. Bwana wangu Yoabu na watumishi wake wote wamepiga kambi mbugani; je ni sawa mimi niende nyumbani nikale na kunywa na kulala na mke wangu? Kama uishivyo na roho yako inavyoishi, sitafanya kitu cha namna hiyo.”

12. Kisha, Daudi akamwambia Uria, “Basi, kaa hapa leo pia, na kesho nitakuacha urudi.” Hivyo Uria akabaki mjini Yerusalemu siku hiyo. Siku iliyofuata,

13. Daudi alimwalika Uria kula na kunywa huko kwake, akamfanya Uria alewe. Hata hivyo, usiku ule Uria hakwenda nyumbani kwake, ila alilala kwenye kochi lake pamoja na watumishi wa bwana wake.

14. Asubuhi yake, Daudi alimwandikia Yoabu barua akampa Uria aipeleke kwa Yoabu.

15. Katika barua hiyo Daudi aliandika hivi: “Mweke Uria kwenye mstari wa mbele, mahali ambako mapigano ni makali kabisa, kisha umwache huko na kurudi nyuma ili apigwe, afe.”

16. Basi, Yoabu alipokuwa anauzingira mji alimweka Uria mahali ambapo alijua wazi wanajeshi wa adui walikuwa hodari sana.

17. Wakazi wa mji huo walitoka katika mji wao na kupigana na Yoabu. Baadhi ya watumishi wa Daudi, waliuawa. Uria Mhiti naye aliuawa pia.

18. Kisha, Yoabu alipeleka habari zote kwa Daudi akimweleza juu ya vita.

19. Yoabu akamwamuru huyo mtumishi aliyemtuma hivi, “Baada ya kumweleza mfalme mambo yote kuhusu vita,

20. akikasirika na kukuuliza, ‘Kwa nini mlikwenda karibu na mji mlipokuwa mnapigana? Hamkujua kwamba wangewapiga mishale kutoka kwenye kuta za mji wao?

21. Nani alimuua Abimeleki mwana wa Yerubeshethi? Si alikuwa mwanamke mmoja mjini Thebesi ambaye alitupa jiwe la kusagia kutoka kwenye ukuta nalo likamuua Abimeleki? Kwa nini basi, mlikwenda karibu na ukuta?’ Basi, wewe utamwambia hivi, ‘Hata mtumishi wako Uria Mhiti, naye amekufa.’”

22. Yule mjumbe alikwenda kwa Daudi na kumwambia yote aliyotumwa na Yoabu ayaseme.

Kusoma sura kamili 2 Samueli 11