Agano la Kale

Agano Jipya

2 Mambo Ya Nyakati 36:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Watu wa Yuda walimtwaa Yehoahazi, mwana wa Yosia, wakamtawaza awe mfalme mahali pa baba yake.

2. Yehoahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitatu alipoanza kutawala; akatawala kwa muda wa miezi mitatu huko Yerusalemu.

3. Baadaye mfalme wa Misri alimwondoa huko Yerusalemu na akaitoza nchi kodi ya kilo 3,400 za fedha na kilo 34 za dhahabu.

4. Kisha mfalme wa Misri akamweka Eliakimu, nduguye Yehoahazi, kuwa mfalme wa Yuda na Yerusalemu, akabadilisha jina lake kuwa Yehoyakimu; lakini Neko akamtwaa Yehoahazi nduguye mpaka Misri.

5. Yehoyakimu alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala, akatawala kwa muda wa miaka kumi na mmoja huko Yerusalemu. Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wake.

6. Nebukadneza mfalme wa Babuloni, alimshambulia, akamfunga kwa pingu ili kumpeleka mateka Babuloni.

7. Nebukadneza pia alitwaa baadhi ya vyombo vya nyumba ya Mwenyezi-Mungu akavipeleka Babuloni na kuviweka katika ikulu yake huko Babuloni.

8. Basi, matendo mengine ya Yehoyakimu, pamoja na machukizo aliyotenda na mengine yaliyoonekana dhidi yake tazama yameandikwa katika Kitabu cha Wafalme wa Israeli na Yuda. Yehoyakini mwanawe alitawala badala yake.

9. Yehoyakini alikuwa na umri wa miaka minane alipoanza kutawala. Alitawala huko Yerusalemu kwa muda wa miezi mitatu na siku kumi. Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu.

10. Mwaka ulipokwisha, mfalme Nebukadneza alituma wajumbe, wakamchukua Yehoyakini mateka hadi Babuloni, pamoja na vyombo vya thamani vya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Akamtawaza Sedekia, nduguye, kuwa mfalme wa Yuda na Yerusalemu.

11. Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja alipoanza kutawala, akatawala huko Yerusalemu kwa muda wa miaka kumi na mmoja.

12. Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, wala hakunyenyekea mbele ya nabii Yeremia ambaye alisema maneno yaliyotoka kwa Mwenyezi-Mungu.

13. Sedekia alimwasi pia mfalme Nebukadneza aliyekuwa amemfanya aape kwa jina la Mungu kwamba hatamwasi. Alikuwa mkaidi sana na mwenye kiburi akakataa kumgeukia Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli.

14. Hata makuhani, viongozi wa Yuda pamoja na watu walikosa uaminifu kabisa wakiiga matendo yote ya kuchukiza ya watu wa mataifa mengine; waliichafua nyumba ya Mwenyezi-Mungu ambayo yeye mwenyewe alikuwa ameitakasa huko Yerusalemu.

Kusoma sura kamili 2 Mambo Ya Nyakati 36