Agano la Kale

Agano Jipya

2 Mambo Ya Nyakati 32:17-32 Biblia Habari Njema (BHN)

17. Mfalme mwenyewe aliandika barua akamtukana na kumdharau Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, akisema, “Kama vile ambavyo miungu ya mataifa mengine haikuweza kuwaokoa watu wao kutoka mikononi mwangu, vivyo hivyo Mungu wa Hezekia hataweza kuwaokoa watu wake.”

18. Maofisa hao waliwaambia kwa sauti kubwa kwa lugha ya Kiebrania watu wa Yerusalemu waliokuwa ukutani, wakikusudia kuwatia hofu na woga ili wauteke mji kwa urahisi.

19. Wakazungumza juu ya Mungu wa Yerusalemu kana kwamba ni miungu ya mataifa mengine; sanamu tu zilizotengenezwa kwa mikono ya wanadamu!

20. Hapo mfalme Hezekia na nabii Isaya, mwana wa Amozi, wakamwomba Mungu na kumlilia awasaidie kwa ajili ya mambo haya.

21. Naye Mwenyezi-Mungu akatuma malaika, akaenda na kuwakatilia mbali mashujaa, wanajeshi, makamanda na maofisa katika kambi ya mfalme wa Ashuru. Basi, mfalme wa Ashuru akarejea nchini mwake amejawa aibu. Mara alipoingia ndani ya nyumba ya mungu wake, baadhi ya wanawe mwenyewe wakamuua papo hapo kwa upanga.

22. Kwa njia hii basi, Mwenyezi-Mungu akamwokoa mfalme Hezekia na wakazi wa Yerusalemu kutoka mkono wa Senakeribu mfalme wa Ashuru, na kutoka mkono wa maadui wake wote. Akawapa maisha ya amani na jirani zake wote.

23. Watu wengi sana walikuja wakamletea Mwenyezi-Mungu tambiko huko Yerusalemu, pia wakamletea Hezekia, mfalme wa Yuda zawadi za thamani. Hivyo kutoka wakati huo, akasifiwa sana na mataifa mengine yote.

24. Wakati huo, Hezekia aliugua sana, karibu na kufa. Akamwomba Mwenyezi-Mungu, naye akamjibu na kumpa ishara.

25. Lakini Hezekia hakumtolea Mwenyezi-Mungu shukrani kwa hayo yote aliyomtendea kwa kuwa moyo wake ulikuwa umejaa majivuno. Hii ilisababisha kutaabika kwa Yuda na Yerusalemu.

26. Kwa hiyo ghadhabu ikawa juu yake, juu ya Yuda na juu ya Yerusalemu. Hatimaye Hezekia alinyenyekea akaacha kuwa na moyo uliojaa majivuno; yeye na wakazi wa Yerusalemu walijinyenyekesha kwa hiyo ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu haikuwajia wakati Hezekia alipokuwa hai.

27. Mfalme Hezekia alitajirika sana, akaheshimiwa. Alijitengenezea hazina za fedha, za dhahabu, za vito, za viungo, ngao na za aina zote za vyombo vya thamani kubwa.

28. Aidha, alijijengea mabohari ya kuhifadhia mazao ya nafaka, divai na mafuta, na mazizi kwa ajili ya ng'ombe na mengine kwa ajili ya kondoo.

29. Vivyo hivyo alijiongezea miji kwa ajili yake mwenyewe, makundi mengi ya ng'ombe na kondoo kwa sababu Mwenyezi-Mungu alimkirimia mali nyingi.

30. Mfalme Hezekia ndiye aliyeyafunga maji ya chemchemi ya Gihoni, akayachimbia mfereji wa chini kwa chini hadi upande wa magharibi wa mji wa Daudi. Hezekia alifaulu katika kila jambo alilofanya,

31. na hata wakati ambapo mabalozi wa wakuu wa Babuloni waliotumwa kwake kuuliza juu ya mambo ya ajabu yaliyotokea humo, Mungu, alimwacha ajiamulie mwenyewe, ili amjaribu na kujua yote yaliyokuwa moyoni mwake.

32. Matendo mengine ya mfalme Hezekia na wema wake, yameandikwa katika Maono ya nabii Isaya mwana wa Amozi, katika Kitabu cha Wafalme wa Yuda na Israeli.

Kusoma sura kamili 2 Mambo Ya Nyakati 32