Agano la Kale

Agano Jipya

2 Mambo Ya Nyakati 29:24-29 Biblia Habari Njema (BHN)

24. Basi, wale makuhani wakawachinja, na kunyunyiza damu yao juu ya madhabahu ili iwe tambiko ya upatanisho kwa Waisraeli wote, kwa maana mfalme Hezekia alikuwa ameagiza itolewe sadaka ya kuteketeza na sadaka ya kuondoa dhambi kwa ajili ya Israeli yote.

25. Mfalme Hezekia aliyafuata maagizo ambayo Mwenyezi-Mungu alikuwa amempa mfalme Daudi kwa njia ya Gadi mwonaji wa mfalme na nabii Nathani. Hivyo basi, akaweka Walawi katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, baadhi yao wakiwa na matoazi, wengine vinanda na wengine vinubi. Hiyo ilikuwa amri ya Mwenyezi-Mungu kwa njia ya manabii wake.

26. Walawi walisimama na vyombo vya muziki vya Daudi, pia makuhani walisimama wakiwa na tarumbeta zao.

27. Basi, Hezekia akaamuru sadaka ya kuteketeza itolewe juu ya madhabahu. Mara tu tambiko hiyo ilipoanza kutolewa, watu walianza kumsifu Mwenyezi-Mungu kwa nyimbo zilizoandamana na mlio wa tarumbeta na vyombo vya muziki vya Daudi mfalme wa Israeli.

28. Watu wote waliokuwamo walishiriki katika ibada. Waimbaji waliendelea kuimba, na tarumbeta zikaendelea kupigwa hadi shughuli za utoaji wa sadaka hiyo ya kuteketeza ilipokamilika.

29. Hatimaye, mfalme Hezekia pamoja na watu wote waliokuwamo waliinama, wakamwabudu Mwenyezi-Mungu.

Kusoma sura kamili 2 Mambo Ya Nyakati 29