Agano la Kale

Agano Jipya

2 Mambo Ya Nyakati 24:3-20 Biblia Habari Njema (BHN)

3. Yehoyada akamwoza wake wawili, nao wakamzalia watoto wa kiume na wa kike.

4. Baadaye Yoashi aliamua kurekebisha nyumba ya Mwenyezi-Mungu.

5. Basi, akawaita makuhani na Walawi na kuwaamuru, “Nendeni katika miji ya Yuda, mkusanye fedha kutoka kwa Waisraeli wote ili kurekebisha nyumba ya Mungu wenu kila mwaka; harakisheni.” Lakini Walawi hawakuharakisha.

6. Basi, mfalme akamwita kiongozi Yehoyada, akamwuliza, “Mbona hujaamrisha Walawi kukusanya kutoka kwa watu wa Yuda na Yerusalemu, kodi ambayo Mose mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, aliagiza watu walipe kwa ajili ya Hema Takatifu la Mwenyezi-Mungu?”

7. (Athalia yule mwanamke mwovu na wafuasi wake walivunja nyumba ya Mungu na kuingia ndani; na vyombo vitakatifu vya nyumba ya Mwenyezi-Mungu walivitumia katika ibada za Mabaali.)

8. Basi, mfalme aliwaamuru Walawi, wakatengeneza sanduku la matoleo na kuliweka nje ya lango la nyumba ya Mwenyezi-Mungu.

9. Kisha tangazo likatolewa kote katika Yuda na Yerusalemu, kwamba watu wote wamletee Mwenyezi-Mungu kodi ambayo Mose mtumishi wa Mungu, aliwaamuru Waisraeli walipokuwa jangwani.

10. Wakuu wote na watu wote walifurahi wakaleta kodi yao wakaitumbukiza kwenye sanduku mpaka walipomaliza kufanya hivyo.

11. Walawi walipopeleka sanduku hilo kwa maofisa wa mfalme, nao walipoona kuwa kuna kiasi kikubwa cha fedha ndani, katibu wa mfalme pamoja na mwakilishi wa kuhani mkuu, walizitoa sandukuni, kisha wakalirudisha mahali pake. Waliendelea kufanya hivyo kila siku, wakakusanya fedha nyingi.

12. Mfalme na Yehoyada walizitoa fedha hizo na kuwapa wale waliosimamia kazi ya urekebishaji wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Nao wakawaajiri waashi, maseremala warekebishe nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Waliajiri pia mafundi wa chuma na shaba ili kurekebisha nyumba ya Mwenyezi-Mungu.

13. Hivyo mafundi hao walishughulika na kazi hiyo kwa bidii, wakairudisha nyumba ya Mwenyezi-Mungu katika hali yake ya awali, wakaiimarisha.

14. Walipomaliza kuitengeneza nyumba ya Mwenyezi-Mungu, walimletea mfalme na Yehoyada dhahabu na fedha iliyobaki; halafu vyombo kwa ajili ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu vilitengenezwa kwa fedha hizo, vyombo hivyo vilikuwa vya kutumika katika huduma ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, matoleo ya sadaka za kuteketeza na mabakuli ya kufukizia ubani, pia vyombo vya dhahabu na vya fedha. Watu waliendelea kutoa sadaka za kuteketezwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu wakati wote wa utawala wa Yehoyada.

15. Lakini Yehoyada alizeeka na alipofikisha umri wa miaka 130, alifariki.

16. Wakamzika katika mji wa Daudi, kwenye makaburi ya wafalme ili kuonesha heshima yao kwake kwa sababu alifanya mema katika Israeli kwa ajili ya Mungu na nyumba yake.

17. Baada ya kifo cha Yehoyada, wakuu wa Yuda walimjia mfalme Yoashi wakamsujudia, wakamshawishi, naye akakubaliana nao.

18. Basi, watu wakaacha kuabudu katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao, wakaanza kuabudu Maashera na sanamu. Ghadhabu ya Mungu iliwaka juu ya Yuda na Yerusalemu kwa sababu ya hatia hii.

19. Hata hivyo, aliwapelekea manabii kuwaonya ili wamrudie Mwenyezi-Mungu, lakini wao hawakuwasikiliza.

20. Ndipo Roho ya Mungu ikamjia Zekaria mwana wa kuhani Yehoyada, naye akasimama mbele ya watu mahali palipokuwa juu kidogo, akawaambia, “Mwenyezi-Mungu aliwaulizeni kwa nini mnazivunja amri zake na sasa hamwezi kufanikiwa! Kwa vile mmemwacha, naye pia amewaacha!”

Kusoma sura kamili 2 Mambo Ya Nyakati 24