Agano la Kale

Agano Jipya

2 Mambo Ya Nyakati 24:15-24 Biblia Habari Njema (BHN)

15. Lakini Yehoyada alizeeka na alipofikisha umri wa miaka 130, alifariki.

16. Wakamzika katika mji wa Daudi, kwenye makaburi ya wafalme ili kuonesha heshima yao kwake kwa sababu alifanya mema katika Israeli kwa ajili ya Mungu na nyumba yake.

17. Baada ya kifo cha Yehoyada, wakuu wa Yuda walimjia mfalme Yoashi wakamsujudia, wakamshawishi, naye akakubaliana nao.

18. Basi, watu wakaacha kuabudu katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao, wakaanza kuabudu Maashera na sanamu. Ghadhabu ya Mungu iliwaka juu ya Yuda na Yerusalemu kwa sababu ya hatia hii.

19. Hata hivyo, aliwapelekea manabii kuwaonya ili wamrudie Mwenyezi-Mungu, lakini wao hawakuwasikiliza.

20. Ndipo Roho ya Mungu ikamjia Zekaria mwana wa kuhani Yehoyada, naye akasimama mbele ya watu mahali palipokuwa juu kidogo, akawaambia, “Mwenyezi-Mungu aliwaulizeni kwa nini mnazivunja amri zake na sasa hamwezi kufanikiwa! Kwa vile mmemwacha, naye pia amewaacha!”

21. Lakini wakamfanyia njama; na kwa amri ya mfalme, wakampiga mawe kwenye ua wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu wakamuua.

22. Mfalme Yoashi aliyasahau mema yote aliyotendewa na Yehoyada, baba yake Zekaria, akamuua mwanawe. Alipokuwa anakufa, alisema, “Mwenyezi-Mungu na ayaone matendo yenu, akalipize kisasi.”

23. Mwishoni mwa mwaka, jeshi la Washamu lilishambulia Yerusalemu na Yuda. Waliwaua wakuu wote, wakateka nyara nyingi na kumpelekea mfalme wa Damasko.

24. Hata ingawa jeshi la Shamu lilikuwa dogo, Mwenyezi-Mungu alilipa ushindi dhidi ya jeshi kubwa la watu wa Yuda kwa sababu hao watu wa Yuda walikuwa wamemwacha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao. Hivyo, Washamu wakatekeleza adhabu ya Mungu juu ya mfalme Yoashi.

Kusoma sura kamili 2 Mambo Ya Nyakati 24