Agano la Kale

Agano Jipya

2 Mambo Ya Nyakati 16:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Katika mwaka wa thelathini na sita wa utawala wa mfalme Asa, Baasha, mfalme wa Israeli, aliishambulia nchi ya Yuda na kuanza kuujenga mji wa Rama ili apate kuzuia mtu yeyote asitoke wala kuingia kwa Asa mfalme wa Yuda.

2. Ndipo mfalme Asa akachukua fedha na dhahabu kutoka katika hazina ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu na ikulu, akazituma Damasko kwa Ben-hadadi, mfalme wa Aramu na ujumbe akasema,

3. “Na tufanye mkataba wa ushirikiano kati yangu na wewe kama walivyofanya baba yangu na baba yako; tazama nakupa zawadi ya fedha na dhahabu; nenda ukavunje mkataba wa ushirikiano ulioko kati yako na mfalme Baasha wa Israeli ili aache mashambulizi dhidi yangu.”

4. Hapo mfalme Ben-hadadi alikubali pendekezo la mfalme Asa, akawatuma majemadari wake na majeshi yake kwenda kuishambulia miji ya Israeli. Nao waliiteka miji ya Iyoni, Dani, Abel-maimu, na miji yote ya Naftali iliyokuwa na ghala za vyakula.

5. Mfalme Baasha alipopata habari za mashambulizi hayo, aliacha kuujenga mji wa Rama, akasimamisha kazi yake.

6. Ndipo mfalme Asa alipowapeleka watu wote wa Yuda, wakahamisha mawe ya Rama na mbao, vifaa ambavyo Baasha alivitumia kujengea. Kisha Asa alitumia vifaa hivyo kujengea miji ya Geba na Mizpa.

7. Wakati huo, Hanani mwonaji alimwendea mfalme Asa wa Yuda, akamwambia, “Kwa sababu ulimtegemea mfalme wa Shamu badala ya kumtegemea Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, jeshi la mfalme wa Shamu limekuponyoka.

Kusoma sura kamili 2 Mambo Ya Nyakati 16