Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 8:35-43 Biblia Habari Njema (BHN)

35. “Mvua isiponyesha kwa sababu wametenda dhambi dhidi yako, wakiomba wakielekea mahali hapa na kulikiri jina lako, pia wakiziacha dhambi zao unapowaonya,

36. tafadhali, uwasikie kutoka huko mbinguni, na usamehe dhambi za watumishi wako, watu wako Israeli, huku ukiwafundisha kufuata njia nyofu; ukanyeshe mvua katika nchi yako hii ambayo uliwapa watu wako iwe mali yako.

37. “Iwapo kuna njaa nchini, au tauni, ukame, ugonjwa wa mimea, nzige au viwavi; au ikiwa watu wako wamezingirwa na adui zao katika mji wao wowote ule; ikiwa kuna pigo lolote au ugonjwa wowote,

38. tafadhali, usikie maombi yoyote yatakayoombwa na watu wako, Israeli, au yatakayoombwa na mtu yeyote au watu wako wote wa Israeli; kila mtu akijua taabu za moyoni mwake, akikuomba huku akinyosha mikono yake kuelekea kwenye nyumba hii.

39. Basi, usikie huko kwako mbinguni, utoe msamaha na kuchukua hatua; pia umtendee kila mtu kadiri anavyostahili (kwani ni wewe tu ujuaye mawazo ya mioyo ya wanadamu wote);

40. ili wakutii wakati wote wanapoishi katika nchi uliyowapa babu zetu.

41. “Vivyo hivyo, wakati mgeni asiye mmoja wa watu wako Israeli akija kutoka nchi ya mbali kwa ajili ya jina lako

42. (maana watu wa mataifa mengine watasikia sifa zako na kuhusu nguvu na uwezo wako), mtu huyo akija na kuomba katika nyumba hii,

43. nakusihi umsikie kutoka huko mbinguni, na umjalie huyo mgeni yote atakayokuomba; kusudi watu wote ulimwenguni wapate kujua jina lako na kukutii kama wafanyavyo watu wako, Israeli, na wapate kufahamu kwamba nyumba hii ambayo nimeijenga, inajulikana kwa jina lako.

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 8