Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 8:25-32 Biblia Habari Njema (BHN)

25. Kwa hiyo, sasa, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, ninakuomba pia utimize ile ahadi uliyomwahidi mtumishi wako, Daudi, baba yangu, ukisema: ‘Siku zote utakuwa na mzawa wa kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli, iwapo wazawa wako watakuwa waangalifu kuhusu mwenendo wao mbele yangu kama wewe ulivyofanya mbele yangu.’

26. Basi, ee Mungu wa Israeli, nakusihi utimize hayo yote uliyomwahidi mtumishi wako, Daudi baba yangu.

27. “Lakini, ee Mungu, kweli utakaa duniani? Ikiwa hata mbingu zenyewe wala mbingu za juu sana hazikutoshi, itakutoshaje nyumba hii ambayo nimeijenga?

28. Hata hivyo, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, mimi mtumishi wako nakuomba unisikie na kunitimizia ombi langu ninaloomba leo.

29. Ichunge nyumba hii usiku na mchana, mahali ambapo umesema, ‘Hapo ndipo watu watakapoliheshimu jina langu;’ unisikie ninapokuja mahali hapa kuomba.

30. Sikia maombi yangu mimi mtumishi wako na ya watu wako Israeli wanapoomba wakielekea mahali hapa. Usikie maombi kutoka huko mbinguni; na ukisha sikia, utusamehe.

31. “Mtu akimkosea mwenzake, naye akaletwa apate kuapa mbele ya madhabahu yako katika nyumba hii, naye akiapa,

32. tafadhali wewe usikie kutoka huko mbinguni, uchukue hatua na kuwahukumu watumishi wako. Aliye na hatia umwadhibu kadiri ya makosa yake, asiye na hatia umwachilie na kumpatia tuzo kadiri ya uadilifu wake.

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 8