Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 8:15-24 Biblia Habari Njema (BHN)

15. akasema, “Atukuzwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwani kwa nguvu yake ametimiza ahadi yake aliyompa baba yangu Daudi, akisema:

16. ‘Tangu niwaondoe watu wangu Israeli nchini Misri, sikuchagua mji wowote katika makabila ya Israeli ili nijengewe nyumba nitakamoabudiwa; ila nilimchagua Daudi, atawale watu wangu, Israeli.’

17. Kwa hiyo, baba yangu alikusudia kujenga nyumba atakamoabudiwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli.

18. Lakini Mwenyezi-Mungu alimwambia baba yangu Daudi, ‘Ni vyema kwamba ulikusudia moyoni mwako kunijengea nyumba.

19. Hata hivyo, si wewe utakayenijengea nyumba, ila mwanao utakayemzaa ndiye atakayenijengea hiyo nyumba.’

20. Na sasa, Mwenyezi-Mungu ametimiza ahadi yake, kwani nimekuwa mfalme mahali pa baba yangu Daudi, na kukikalia kiti cha enzi cha Israeli kama Mwenyezi-Mungu alivyoahidi; pia nimejenga nyumba ya kumwabudia Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli.

21. Zaidi ya hayo, nimetenga mahali pa kuweka sanduku la agano ambalo ndani yake mna agano alilofanya Mwenyezi-Mungu na babu zetu, wakati alipowatoa katika nchi ya Misri.”

22. Kisha Solomoni alisimama mbele ya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu, naye, akiwa mbele ya jumuiya yote ya Waisraeli, aliinua mikono yake juu,

23. akasema, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu mwingine kama wewe, juu mbinguni, ama chini duniani! Wewe u mwaminifu, kwani umetimiza agano lako na kuwaonesha fadhili zako watumishi wako wanaoishi wakikutii kwa moyo wao wote.

24. Umetimiza ahadi uliyoitoa kwa mtumishi wako Daudi baba yangu; naam, yale uliyonena umeyatimiza leo kwa uwezo wako mwenyewe.

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 8