Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 21:7-22 Biblia Habari Njema (BHN)

7. Hapo, Yezebeli, mkewe, akamwambia, “Anayetawala Israeli ni nani? Si ni wewe? Amka, ule na uchangamke; mimi binafsi nitakupa shamba la mizabibu la Nabothi, Myezreeli.”

8. Basi, Yezebeli akaandika barua kadha kwa jina la Ahabu na kuzipiga mhuri wa mfalme. Kisha akapeleka barua hizo kwa wazee na watu mashuhuri walioishi na Nabothi huko mjini.

9. Barua zenyewe ziliandikwa hivi: “Pigeni mbiu ya mfungo, mkutane na kumpa Nabothi mahali pa heshima kati ya watu.

10. Kisha, tafuteni walaghai wawili wamkabili na kumshtaki wakisema: ‘Wewe umemwapiza Mungu na mfalme.’ Kisha mtoeni nje, mkamuue kwa kumpiga mawe!”

11. Basi, wakazi wenzake Nabothi, wazee na watu mashuhuri wa mji wa Yezreeli, wakafanya kama Yezebeli alivyowaagiza. Kwa mujibu wa barua aliyowapelekea,

12. wakapiga mbiu ya mfungo, wakakutana na kumweka Nabothi mahali pa heshima kati ya watu.

13. Wale walaghai wawili wakaketi kumkabili Nabothi, kisha wakamshtaki hadharani wakisema, “Nabothi amemwapiza Mungu na mfalme.” Basi, Nabothi akatolewa nje ya mji, akauawa kwa kupigwa mawe.

14. Kisha, Yezebeli akapelekewa habari kwamba Nabothi amekwisha uawa kwa kupigwa mawe.

15. Mara tu Yezebeli alipopata habari kwamba Nabothi amekwisha uawa kwa kupigwa mawe, akamwambia Ahabu, “Inuka! Nenda ukamiliki lile shamba la mizabibu la Nabothi, Myezreeli, ambalo alikataa kukuuzia. Nabothi hayuko hai tena; amekwisha fariki.”

16. Mara tu Ahabu aliposikia Nabothi amekwisha fariki, aliinuka kwenda kulimiliki shamba la mizabibu la Nabothi.

17. Basi, neno la Mwenyezi-Mungu likamjia nabii Elia wa Tishbe:

18. “Inuka uende kukutana na Ahabu mfalme wa Israeli, ambaye yuko Samaria. Utamkuta katika shamba la mizabibu la Nabothi, akilimiliki.

19. Mwambie, Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Umeua na kumiliki pia?’ Mwambie Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Mahali pale mbwa walipoiramba damu ya Nabothi, ndipo watakapoilamba damu yako.’”

20. Basi, Ahabu alipomwona Elia, akasema, “Ewe adui yangu, umenifuma?” Elia akamjibu, “Naam! Nimekufuma, kwa sababu wewe umenuia kabisa kutenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu.

21. Haya! Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Hakika, nitakuletea maangamizi. Nitakuzoa wewe na kufutilia mbali kila mwanamume wa ukoo wako katika Israeli, awe mtumwa au huru.

22. Jamaa yako nitaifanya kama jamaa ya Yeroboamu, mwana wa Nebati, na kama jamaa ya Baasha mwana wa Ahiya, kwa sababu umeiwasha hasira yangu na kuwafanya watu wa Israeli watende dhambi.’

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 21