Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 16:6-21 Biblia Habari Njema (BHN)

6. Hatimaye, Baasha alifariki, akazikwa huko Tirza; mwanawe Ela akatawala mahali pake.

7. Tena neno la Mwenyezi-Mungu dhidi ya Baasha na jamaa yake, lilimjia Yehu mwanawe Hanani kwa sababu ya maovu aliyotenda mbele ya Mwenyezi-Mungu. Baasha alimkasirisha Mwenyezi-Mungu kwa matendo yake; alimwiga Yeroboamu na jamaa yake na kuiletea jamaa yake maangamizi.

8. Mnamo mwaka wa ishirini na sita wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Ela mwana wa Baasha, alianza kutawala huko Israeli kutoka Tirza. Alitawala kwa muda wa miaka miwili.

9. Mtumishi wake Zimri ambaye alisimamia nusu ya kikosi cha magari yake ya kukokotwa, alikula njama juu yake. Siku moja, mfalme Ela alipokuwa huko Tirza nyumbani kwa Arsa aliyekuwa msimamizi wa ikulu, alikunywa, akalewa.

10. Basi, Zimri akaingia ndani, akamuua. Kisha akatawala mahali pake. Huu ulikuwa mwaka wa ishirini na saba wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda.

11. Mara tu alipoanza kutawala, Zimri aliwaua watu wote wa jamaa ya Baasha; hakumwachia hata mwanamume mmoja wa jamaa yake wala wa rafiki zake;

12. ikawa kama alivyosema Mwenyezi-Mungu dhidi ya Baasha, kwa njia ya nabii Yehu.

13. Mambo haya yalifanyika kwa sababu ya dhambi alizotenda Baasha na mwanawe Ela. Walimkasirisha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa kutenda dhambi na kuwafanya watu wa Israeli watende dhambi kwa sanamu za miungu yao.

14. Matendo mengine ya Ela, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Israeli.

15. Zimri alitawala huko Israeli kutoka Tirza kwa muda wa siku saba. Huo ulikuwa mwaka wa ishirini na saba wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda. Basi, watu wa Israeli walikuwa wamepiga kambi kuuzingira mji wa Gibethoni wa Wafilisti,

16. na majeshi ya watu wa Israeli waliposikia kwamba Zimri alikuwa amekula njama, akamuua mfalme, wote wakamtawaza Omri, amiri jeshi wao, kuwa mfalme wa Israeli siku hiyohiyo.

17. Omri na majeshi yake akaondoka Gibethoni, akaenda na kuuzingira mji wa Tirza.

18. Zimri alipoona kwamba mji umezingirwa, aliingia ngomeni, ndani ya ikulu, akaichoma moto, naye akafia humo.

19. Jambo hilo lilifanyika kwa sababu ya dhambi alizotenda alifanya maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, akamwiga Yeroboamu na kuwafanya watu wa Israeli watende dhambi.

20. Matendo mengine ya Zimri na njama aliyokula, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Israeli.

21. Watu wa Israeli, sasa, waligawanyika makundi mawili: Kundi moja lilimtambua Tibni mwana wa Ginathi kuwa mfalme, na kundi la pili lilimtambua Omri.

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 16