Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 13:10-27 Biblia Habari Njema (BHN)

10. Basi, mtu huyo akaenda zake, wala hakurudi kwa njia ile aliyoijia Betheli.

11. Wakati huo, palikuwa na nabii mmoja mzee huko Betheli. Wanawe wakamwendea, wakamweleza mambo yote aliyotenda yule mtu wa Mungu siku hiyo, huko Betheli; wakamwambia pia yale maneno yule mtu aliyomwambia mfalme Yeroboamu.

12. Baba yao akawauliza, “Amefuata njia ipi?” Nao wakamwonesha njia aliyoifuata huyo mtu wa Mungu kutoka Yuda.

13. Naye akawaambia watoto wake, “Nitandikieni huyo punda.” Nao wakamtandikia punda, na mzee akapanda juu yake.

14. Akamfuata yule mtu wa Mungu, akamkuta ameketi chini ya mti wa mwaloni. Basi, akamwuliza, “Je, wewe ndiwe yule mtu wa Mungu kutoka Yuda?” Naye akamjibu, “Naam! Mimi ndiye.”

15. Huyo mzee akamwambia, “Karibu nyumbani kwangu, ukale chakula.”

16. Lakini yeye akamwambia, “Siwezi kurudi pamoja nawe, wala kuingia nyumbani kwako. Siwezi kula chakula au kunywa maji mahali hapa,

17. maana, Mwenyezi-Mungu aliniamuru nisile chakula au kunywa maji mahali hapa, wala nisirudi kwa njia niliyoijia.”

18. Huyo mzee wa Betheli akamwambia, “Mimi pia ni nabii kama wewe, na Mwenyezi-Mungu amenena nami kwa njia ya malaika akisema, ‘Mrudishe nyumbani kwako, ale chakula na kunywa maji.’” Lakini huyo nabii mzee alikuwa anamdanganya tu.

19. Basi, mtu wa Mungu akarudi pamoja naye, akala chakula na kunywa maji kwa huyo mzee.

20. Walipokuwa mezani, neno la Mwenyezi-Mungu likamjia huyo nabii mzee,

21. naye akamwambia kwa sauti huyo mtu wa Mungu kutoka Yuda: “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Wewe umeacha kutii ujumbe wa Mwenyezi-Mungu; wewe hukufuata amri aliyokupa Mwenyezi-Mungu, Mungu wako.

22. Badala yake, umerudi hapa, ukala chakula na kunywa maji mahali hapa ambapo uliambiwa usile chakula wala kunywa maji. Basi, mwili wako hautazikwa kwenye kaburi la babu zako.’”

23. Walipomaliza kula, huyo nabii mzee akamtandikia punda huyo mtu wa Mungu, naye akaondoka.

24. Alipokuwa anakwenda zake, simba akakutana naye njiani, akamuua; mwili wake ukawa umetupwa hapo barabarani; punda wake na huyo simba wakawa wamesimama kando yake.

25. Watu waliopitia hapo na kuiona maiti barabarani, na simba amesimama karibu nayo, wakaenda mpaka mjini alimokuwa anakaa yule nabii, wakawaambia watu.

26. Nabii yule ambaye alikuwa amemkaribisha nyumbani kwake aliposikia habari hiyo, akasema, “Huyo ni yuleyule mtu wa Mungu aliyekataa kutii neno la Mwenyezi-Mungu! Mwenyezi-Mungu amemtuma simba, akamshambulia na kumwua kama alivyokuwa amemwambia.”

27. Hapo akawaambia wanawe “Nitandikie punda.” Nao wakamtandikia.

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 13