Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 10:15-25 Biblia Habari Njema (BHN)

15. Kiasi hicho si pamoja na dhahabu aliyopata kwa wafanyabiashara na wachuuzi, kwa wafalme wote wa Arabia na wakuu wa mikoa ya Israeli.

16. Mfalme Solomoni alitengeneza ngao kubwa 200 kwa dhahabu iliyofuliwa; kila ngao kilo 7 za dhahabu.

17. Alitengeneza ngao ndogondogo 300 kwa dhahabu iliyofuliwa, kila ngao kilo 1.5; halafu mfalme akaziweka katika jengo lililoitwa Nyumba ya Msitu wa Lebanoni.

18. Vilevile mfalme alitengeneza kiti cha enzi kikubwa cha pembe, akakipaka dhahabu safi kabisa.

19. Kiti hicho kilikuwa na ngazi sita. Sehemu ya juu ilikuwa imeviringwa na kiliwekewa mahali pa kuegemeza mkono pande zake mbili; na sanamu za simba wawili zimesimama moja kando ya mahali hapo pa kuegemeza mkono.

20. Kulikuwa pia na sanamu kumi na mbili za simba zimesimama, moja mwishoni mwa kila ngazi. Kiti kama hicho hakijawahi kutengenezwa katika ufalme wowote ule.

21. Vyombo vyote vya kunywea divai vya mfalme Solomoni vilikuwa vya dhahabu, na vyombo vyote vilivyokuwa katika Nyumba ya Msitu wa Lebanoni vilikuwa vya dhahabu safi; hakuna kilichotengenezwa kwa madini ya fedha kwani madini ya fedha haikuthaminiwa kuwa kitu wakati huo.

22. Kwa kuwa mfalme Solomoni alikuwa na msafara wa meli za Tarshishi zilizokuwa zikisafiri pamoja na meli za Hiramu, kila mwaka wa tatu meli hizo za Tarshishi zilimletea mfalme dhahabu, fedha, pembe, nyani na tausi.

23. Hivyo, mfalme Solomoni aliwapita wafalme wote duniani kwa mali na hekima.

24. Watu wa nchi zote walikuwa na hamu ya kumwendea Solomoni ili kusikiliza hekima yake ambayo Mungu alikuwa amemjalia.

25. Kila mmoja wao alimletea zawadi: Vyombo vya fedha, vya dhahabu, mavazi, manemane, manukato, farasi na nyumbu. Zawadi hizi alizipokea kila mwaka.

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 10