Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 1:8-26 Biblia Habari Njema (BHN)

8. Lakini kuhani Sadoki, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na nabii Nathani na Shimei, Rei pamoja na walinzi wa Daudi, hawakumuunga mkono Adoniya.

9. Siku moja, Adoniya alitoa sadaka ya kondoo, ng'ombe na ndama wanono kwenye Jiwe la Nyoka, karibu na chemchemi iitwayo Enrogeli. Akawaalika kwenye karamu ya sadaka hiyo ndugu zake wote, yaani wana wengine wa mfalme, na watumishi wote wa mfalme waliokuwa wa kabila la Yuda.

10. Lakini, nabii Nathani, Benaya, walinzi wa mfalme na Solomoni ndugu yake hakuwaalika.

11. Hapo, Nathani akamwendea Bathsheba mama yake Solomoni, akamwuliza, “Je, hujasikia kwamba Adoniya, mwanawe Hagithi, amejinyakulia mamlaka ya ufalme na bwana wetu Daudi hana habari?

12. Basi, kama ukitaka kuyaokoa maisha yako na ya mwanao Solomoni, nakushauri hivi:

13. Mwendee mfalme Daudi, umwulize, ‘Je, bwana wangu mfalme, hukuniapia mimi mtumishi wako ukisema, “Mwana wako Solomoni atatawala mahali pangu na atakaa juu ya kiti changu cha enzi?” Imekuwaje basi, sasa Adoniya anatawala?’

14. Na utakapokuwa bado unaongea na mfalme, mimi nitaingia na kuyathibitisha maneno yako.”

15. Basi, Bathsheba alimwendea mfalme chumbani mwake (wakati huo mfalme alikuwa mzee sana, naye Abishagi, Mshunami alikuwa akimhudumia).

16. Bathsheba aliinama, akamsujudia mfalme, naye mfalme akamwuliza, “Unataka nini?”

17. Bathsheba akamjibu, “Bwana wangu, uliniapia mimi mtumishi wako mbele ya Bwana Mungu wako, ukisema: ‘Mwana wako Solomoni atatawala baada yangu, na ataketi juu ya kiti changu cha enzi.’

18. Sasa, tazama, Adoniya anatawala ingawa wewe bwana wangu mfalme hujui kuhusu hayo.

19. Ametoa sadaka ya ng'ombe, ya vinono, na kondoo wengi, na kuwaita wana wote wa mfalme, kuhani Abiathari, na Yoabu jemadari wa jeshi, lakini mtumishi wako Solomoni hakumkaribisha.

20. Na sasa, bwana wangu mfalme, Waisraeli wote wanakungojea, ili uwaambie yule atakayeketi juu ya kiti chako baada yako, bwana wangu mfalme.

21. La sivyo, itatokea ya kwamba, wakati ambapo wewe bwana wangu, mfalme, utakapofariki mimi pamoja na mwanangu Solomoni tutahesabika kama wenye hatia.”

22. Wakati Bathsheba alipokuwa akizungumza na mfalme, nabii Nathani aliingia ikulu.

23. Nao watu wakamwambia mfalme, “Nabii Nathani yuko hapa.” Naye alipomfikia mfalme, alimwinamia mfalme mpaka uso ukafika chini udongoni.

24. Ndipo Nathani aliposema, “Bwana wangu, je, ulisema, ‘Adoniya atatawala baada yangu na atakaa juu ya kiti changu cha enzi?’

25. Kwa maana leo ameteremka, akatoa sadaka ya ng'ombe, vinono na kondoo wengi na amewakaribisha wana wa mfalme, Yoabu jemadari wa jeshi, na kuhani Abiathari, na, tazama, wanakula na kunywa mbele yake, na kusema, ‘Uishi mfalme Adoniya!’

26. Lakini hakunialika mimi, mtumishi wako wala kuhani Sadoki, wala Benaya mwana wa Yehoyada na mtumishi wako Solomoni.

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 1