Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 9:10-24 Biblia Habari Njema (BHN)

10. Shauli akamjibu, “Hilo ni jambo jema; haya, twende.” Hivyo, wakaenda kwenye mji alimokuwa anakaa yule mtu wa Mungu.

11. Walipokuwa wanapanda mlima kuelekea mjini, wakakutana na wasichana waliokuwa wakienda kuteka maji. Wakawauliza wasichana hao, “Je, mwonaji yuko mjini?”

12. Wale wasichana wakawajibu, “Ndiyo, yuko. Tena yuko mbele yenu; mkifanya haraka mtamkuta. Ameingia tu mjini leo, kwa sababu leo watu watatambika huko mlimani.

13. Mara mtakapoingia mjini, mtamkuta kabla hajaenda mahali pa ibada mlimani ili kula. Maana watu hawatakula mpaka kwanza yeye abariki tambiko. Baadaye wale walioalikwa watakula. Hivyo nendeni haraka; mtakutana naye mara.”

14. Hivyo Shauli na mtumishi wake walikwenda mjini. Walipokuwa wanaingia mjini, walimwona Samueli akitoka mjini, na anaelekea mahali pa juu.

15. Jana yake, kabla Shauli hajafika mjini hapo, Mwenyezi-Mungu alikuwa amemwambia hivi Samueli:

16. “Kesho, wakati kama huu, nitakuletea mtu kutoka nchi ya kabila la Benyamini, nawe utampaka mafuta kuwa mtawala wa watu wangu Israeli. Yeye atawaokoa watu wangu kutoka kwa Wafilisti, kwani nimeyaona mateso ya watu wangu na kilio chao kimenifikia.”

17. Samueli alipomwona tu Shauli, Mwenyezi-Mungu alimwambia, “Huyu ndiye yule mtu niliyekuambia. Yeye ndiye atakayewatawala watu wangu.”

18. Hapo Shauli alimwendea Samueli aliyekuwa karibu na lango la mji na kumwuliza, “Nakuomba unioneshe nyumba ya mwonaji.”

19. Samueli akamjibu; “Mimi ndiye mwonaji. Nitangulieni kwenda mahali pa juu kwani leo mtakula pamoja nami. Kesho asubuhi maswali yote uliyo nayo nitayajibu.

20. Kuhusu wale punda waliopotea siku tatu zilizopita, msiwe na wasiwasi juu yao; wamekwisha patikana. Lakini ni nani yule ambaye Waisraeli wanamtaka sana? Je, si wewe na jamaa yote ya baba yako?”

21. Shauli akajibu: “Mimi ni wa kabila la Benyamini, kabila dogo kuliko makabila yote ya Israeli. Na katika kabila lote la Benyamini jamaa yangu ndiyo ndogo kabisa. Lakini, kwa nini unanizungumzia namna hiyo?”

22. Kisha Samueli akampeleka Shauli na mtumishi wake sebuleni, akawapa mahali pa heshima, ambako wageni walioalikwa walikuwa wamekaa. Kulikuwa na wageni wapatao thelathini.

23. Samueli akamwambia mpishi, “Lete ile sehemu niliyokupatia, nikakuambia uiweke kando.”

24. Yule mpishi akaenda akaleta paja na sehemu ya nyama iliyokuwa upande wa juu wa paja hilo na kuviweka mbele ya Shauli. Ndipo Samueli akamwambia Shauli, “Tazama kile ulichowekewa; sasa kimewekwa mbele yako. Sasa ule kwa sababu kimewekwa kwa ajili yako ili upate kula pamoja na wageni.”Hivyo, Shauli akala pamoja na Samueli siku hiyo.

Kusoma sura kamili 1 Samueli 9