Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 7:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Kisha, watu wa Kiriath-yearimu wakaenda na kulichukua sanduku la Mwenyezi-Mungu, wakalipeleka nyumbani kwa Abinadabu, aliyeishi milimani. Wakamweka wakfu mtoto wake wa kiume aliyeitwa Eleazari ili alitunze sanduku hilo.

2. Tangu sanduku la Mwenyezi-Mungu lipelekwe mjini Kiriath-yearimu muda mrefu ulipita, miaka ishirini hivi. Wakati huo Waisraeli wote walimlilia Mwenyezi-Mungu.

3. Samueli akawaambia Waisraeli, “Kama mnamrudia Mwenyezi-Mungu kwa moyo wenu wote, ni lazima mwondoe kati yenu miungu ya kigeni na sanamu za Ashtarothi. Mwelekeeni Mwenyezi-Mungu kwa moyo wote, na kumtumikia yeye peke yake; naye atawaokoa kutoka mikononi mwa Wafilisti.”

4. Hivyo, Waisraeli wakatupilia mbali sanamu za Mabaali na Maashtarothi, wakamtumikia Mwenyezi-Mungu peke yake.

5. Kisha, Samueli akawaita Waisraeli wote wakutane huko Mizpa, akawaambia, “Huko nitamwomba Mwenyezi-Mungu kwa ajili yenu.”

6. Hivyo, Waisraeli wote wakakusanyika huko Mizpa. Walichota maji na kuyamimina mbele ya Mwenyezi-Mungu, wakafunga siku ile yote na kusema, “Tumetenda dhambi mbele ya Mwenyezi-Mungu.” (Samueli alikuwa mwamuzi wa Waisraeli huko Mizpa).

7. Wafilisti waliposikia kuwa Waisraeli wamekusanyika huko Mizpa, wakuu watano wa Wafilisti wakaenda kuwashambulia. Waisraeli waliposikia juu ya jambo hilo waliwaogopa Wafilisti.

8. Basi, wakamwambia Samueli, “Usiache kumlilia Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kwa ajili yetu. Endelea kumlilia atuokoe kutoka kwa Wafilisti.”

9. Kwa hiyo Samueli alichukua mwanakondoo anayenyonya akamtolea Mwenyezi-Mungu kama sadaka ya kuteketezwa nzima. Kisha Samueli akamlilia Mwenyezi-Mungu kwa ajili ya Israeli, naye akajibu kilio chake.

10. Samueli alipokuwa anatoa ile sadaka ya kuteketezwa, Wafilisti walikaribia kuwashambulia Waisraeli. Lakini Mwenyezi-Mungu akatoa sauti kubwa ya ngurumo dhidi ya Wafilisti, na kuwavuruga Wafilisti, nao wakatimuliwa mbele ya Waisraeli.

Kusoma sura kamili 1 Samueli 7