Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 30:9-22 Biblia Habari Njema (BHN)

9. Kwa hiyo, Daudi akaondoka pamoja na wale watu 600 aliokuwa nao. Walipofika kwenye kijito cha Besori, wakawakuta baadhi ya watu waliotekwa wameachwa hapo.

10. Lakini Daudi aliendelea kulifuatilia lile genge akiwa na watu 400, watu 200 wakabaki hapo kwani walichoka mno, wasiweze kuvuka kijito hicho.

11. Wale watu waliokuwa na Daudi walimkuta mtu mmoja Mmisri nyikani, nao wakampeleka kwa Daudi. Wakampa mtu huyo mkate na maji.

12. Pia walimpa kipande cha mkate wa tini na vishada viwili vya zabibu kavu. Alipomaliza kula, akapata nguvu, kwani alikuwa hajala wala kunywa kitu chochote kwa muda wa siku tatu, mchana na usiku.

13. Daudi akamwuliza, “Bwana wako ni nani? Na umetoka wapi?” Yeye akamwambia, “Mimi ni kijana Mmisri. Ni mtumishi wa Mmaleki mmoja. Bwana wangu aliniacha nyuma siku tatu zilizopita kwa kuwa nilikuwa mgonjwa.

14. Sisi tulishambulia sehemu ya jangwa wanamoishi Wakerethi, eneo la Yuda pamoja na sehemu ya jangwa unakoishi ukoo wa Kalebu, tukauteketeza kwa moto mji wa Siklagi.”

15. Daudi akamwuliza, “Je, utaweza kunipeleka kwenye genge hilo?” Kijana akamjibu, “Ikiwa utaniapia kwa jina la Mungu kuwa hutaniua, wala kunitia mikononi mwa bwana wangu, nitakupeleka.”

16. Yule kijana alimwongoza Daudi hadi genge lile lilipokuwa. Walipofika huko waliwakuta wateka nyara hao wakiwa wametawanyika kila mahali kwani walikuwa wakila na kunywa kwa sababu nyara walizoteka kutoka nchi ya Wafilisti na nchi ya Yuda zilikuwa nyingi sana.

17. Daudi aliwapiga tangu asubuhi hadi siku ya pili jioni. Hakuna mwanamume yeyote aliyenusurika isipokuwa vijana 400 ambao walipanda ngamia na kukimbia.

18. Daudi aliokoa kila kitu Waamaleki walichokuwa wamekiteka, hata na wake zake wawili.

19. Chochote kilichokuwa chao, kiwe kikubwa au kidogo, mtoto wa kiume au wa kike, Daudi alikikomboa.

20. Pia Daudi aliyarudisha makundi yote ya kondoo na ng'ombe, na watu wake wakawa wanaswaga wanyama hao wakiwatanguliza mbele ya wanyama wale wengine wakisema, “Nyara za Daudi.”

21. Daudi akawarudia wale watu 200 ambao waliachwa kwenye kijito cha Besori kwa sababu walikuwa wamechoka kumfuata. Wale watu walipomwona Daudi pamoja na wale waliokuwa pamoja naye, wakaenda kumlaki. Daudi alipofika karibu na watu hao, akawasalimu.

22. Lakini watu wote waovu na baradhuli miongoni mwa watu waliofuatana na Daudi, wakasema, “Hatutawapa watu hawa nyara zozote tulizozikomboa kwani hawakwenda pamoja nasi. Ila wawachukue wake zao na watoto wao, waende zao.”

Kusoma sura kamili 1 Samueli 30