Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 23:10-24 Biblia Habari Njema (BHN)

10. Kisha Daudi akaomba, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa hakika mimi mtumishi wako, nimesikia kwamba Shauli anapanga kuja kuangamiza mji wa Keila kwa sababu yangu.

11. Je, wakazi wa Keila watanitia mikononi mwa Shauli? Je, Shauli atakuja kweli kama nilivyosikia mimi mtumishi wako? Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nakuomba unijibu mimi mtumishi wako.”Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Shauli atakuja.”

12. Daudi akamwuliza, “Je, wakazi wa Keila watanitia mikononi mwa Shauli, mimi pamoja na watu wangu?” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Watakutia mikononi mwake.”

13. Kisha, Daudi na watu wake ambao walikuwa kama 600, waliondoka na kwenda popote walipoweza kwenda. Shauli aliposikia kwamba Daudi amekwisha kimbia kutoka Keila, akaiacha mipango yake yote.

14. Basi, Daudi alibaki ngomeni jangwani, katika nchi ya milima ya mbuga za Zifu. Shauli alimtafuta kila siku, lakini Mungu hakumtia Daudi mikononi mwa Shauli.

15. Daudi alijua kuwa Shauli alitaka kuyaangamiza maisha yake. Daudi akawa katika mbuga za Zifu, huko Horeshi.

16. Yonathani mwana wa Shauli alimfuata Daudi huko Horeshi akamtia moyo kwamba Mungu anamlinda.

17. Yonathani alimwambia, “Usiogope, baba yangu Shauli hatakupata. Wewe utakuwa mfalme wa Israeli, mimi nitakuwa wa pili wako. Hata Shauli baba yangu anajua jambo hili.”

18. Hao wote wawili, wakafanya agano mbele ya Mwenyezi-Mungu. Daudi akabaki mjini Horeshi na Yonathani akaenda zake nyumbani.

19. Shauli alipokuwa bado huko Gibea, Wazifu wakamwendea na kumwambia, “Daudi anajificha katika nchi yetu kwenye ngome huko Horeshi, kwenye mlima Hakila, ulio upande wa kusini wa Yeshimoni.

20. Sasa, mfalme, njoo ili utekeleze yaliyomo moyoni mwako, na kwa upande wetu, jukumu letu litakuwa kumtia Daudi mikononi mwako.”

21. Shauli akawajibu, “Nyinyi kweli mnanionea huruma; Mwenyezi-Mungu na awabariki.

22. Nendeni, mkahakikishe tena, mjue mahali anapojificha, na ni nani amemwona mahali hapo; maana nimeambiwa kwamba yeye ni mjanja sana.

23. Chunguzeni kila upande mjue mahali anapojificha, kisha mniletee habari kamili. Halafu nitakwenda pamoja nanyi na ikiwa bado atakuwa yuko huko, basi, mimi nitamsaka miongoni mwa maelfu yote ya watu wa Yuda.”

24. Basi, wakaondoka kwenda Zifu, wakimtangulia Shauli.Wakati huo, Daudi na watu wake walikuwa katika jangwa la Maoni, katika bonde la Araba kusini mwa Yeshimoni.

Kusoma sura kamili 1 Samueli 23