Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 20:30-42 Biblia Habari Njema (BHN)

30. Hapo Shauli akawaka hasira dhidi ya Yonathani, akamwambia, “Mwana wa mwanamke mpotovu na mwasi wewe! Ninajua kuwa umejichagulia mwana wa Yese kwa aibu yako mwenyewe, na kumwaibisha mama yako!

31. Je, hujui kwamba Daudi awapo hai, wewe hutaweza kupata fursa ya kuwa mfalme wa nchi hii? Sasa nenda ukamlete hapa kwangu, kwa kuwa lazima auawe.”

32. Yonathani akamjibu, “Kwa nini auawe? Amefanya nini?”

33. Lakini Shauli mara akamtupia Yonathani mkuki ili amuue. Naye Yonathani akatambua kuwa baba yake alikuwa amepania kumwua Daudi.

34. Hapo Yonathani, huku akiwa amekasirika sana, aliondoka mezani kwa haraka, wala hakula chakula chochote siku hiyo ya pili ya sherehe za mwezi mwandamo. Yonathani alihuzunika sana juu ya Daudi kwa sababu baba yake alikuwa amemwaibisha.

35. Kesho yake asubuhi, Yonathani alikwenda kule shambani, kukutana na Daudi kama walivyoagana. Alikwenda huko na kijana mmoja wa kiume.

36. Alipofika huko alimwambia yule kijana wake, “Kimbia ukaitafute mishale ambayo nitapiga.” Yule kijana alipokuwa anakimbia, Yonathani akapiga mshale mbele yake.

37. Yule kijana alipofika mahali ambapo mshale uliangukia, Yonathani akamwita, “Mshale uko mbele yako.

38. Fanya haraka na usisimame tu mahali hapo.” Yule kijana alikusanya mishale na kumwendea bwana wake.

39. Lakini yule kijana hakujua chochote juu ya maana ya kitendo hicho. Waliojua ni Yonathani na Daudi tu.

40. Yonathani akamkabidhi yule kijana silaha zake na kumwambia “Nenda urudi mjini.”

41. Mara yule kijana alipokwisha ondoka, Daudi akainuka na kutoka mahali alipojificha karibu na rundo la mawe. Aliinama chini kwa heshima mara tatu mbele ya Yonathani. Wote wawili, Daudi na Yonathani, wakakumbatiana na kulia. Daudi alikuwa na uchungu zaidi kuliko Yonathani.

42. Halafu Yonathani akamwambia Daudi, “Nenda kwa amani. Tumekwisha apa wote kwa jina la Mwenyezi-Mungu, kuwa Mwenyezi-Mungu awe shahidi kati yetu milele, na kati ya wazawa wangu na wazawa wako milele.” Daudi akainuka na kwenda zake, naye Yonathani akarudi mjini.

Kusoma sura kamili 1 Samueli 20