Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 18:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Shauli alipomaliza kuzungumza na Daudi, Yonathani mwana wa Shauli, alivutiwa sana na Daudi, akampenda kwa moyo wake wote kama alivyojipenda yeye mwenyewe.

2. Tangu siku hiyo, Shauli akamchukua Daudi nyumbani kwake, asimruhusu kurudi nyumbani kwa baba yake.

3. Kwa kuwa Yonathani alimpenda Daudi kama roho yake, alifanya agano naye.

4. Alivua vazi alilovaa na kumpa Daudi pamoja na silaha zake, hata upanga, upinde na mkanda wake.

5. Kokote Daudi alikotumwa na Shauli, Daudi alifanikiwa. Hivyo, Shauli akamfanya kuwa mkuu wa jeshi lake. Jambo hilo liliwafurahisha watu wote hata watumishi wa Shauli.

6. Askari walipokuwa wanarudi nyumbani, pamoja na Daudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake kutoka kila mji katika Israeli walitoka kwenda kumlaki mfalme Shauli. Wanawake nao walikuwa wanaimba nyimbo za furaha, wakipiga matari na vinubi.

7. Pia walikuwa wanacheza na kuimba nyimbo za kuitikiana hivi:“Shauli ameua maelfu yake,na Daudi ameua makumi elfu yake.”

8. Shauli hakupendezwa na maneno ya wimbo huo, hivyo akakasirika sana. Akasema, “Wamempa Daudi makumi elfu, lakini mimi wamenipa maelfu tu. Lililobakia ni kumpa Daudi ufalme.”

9. Tangu siku hiyo, Shauli akawa anamwonea kijicho Daudi.

10. Kesho yake, roho mwovu kutoka kwa Mungu, alimvamia Shauli kwa ghafla, akawa anapayukapayuka kama mwendawazimu nyumbani kwake. Daudi alikuwa anapiga kinubi kama alivyofanya siku zote. Shauli alikuwa na mkuki mkononi mwake;

11. basi, alimtupia Daudi mkuki mara mbili kwani alifikiri, “Nitambana Daudi ukutani.” Lakini Daudi alikwepa mara zote mbili.

Kusoma sura kamili 1 Samueli 18