Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 17:39-48 Biblia Habari Njema (BHN)

39. Daudi akajifunga upanga wa Shauli, akajaribu kutembea; lakini akashindwa kwa kuwa hakuyazoea mavazi kama hayo. Akamwambia Shauli, “Siwezi kwenda vitani nikiwa nimevaa mavazi haya, kwani mimi sijayazoea.” Kwa hiyo, akayavua.

40. Daudi akachukua fimbo yake mkononi, akajichagulia mawe matano mazuri kutoka kwenye kijito, akayatia katika mfuko wake wa mchungaji. Kombeo lake likiwa tayari mkononi mwake, akaanza kumwendea Goliathi Mfilisti.

41. Yule Mfilisti, naye akaanza kumwendea Daudi, na yule aliyemchukulia ngao yake akiwa mbele yake.

42. Yule Mfilisti alipoangalia na kumwona vizuri Daudi, alimdharau, kwani Daudi alikuwa kijana tu, mwenye afya na wa kupendeza.

43. Goliathi akamwuliza Daudi, “Sasa, hiyo fimbo ni ya nini? Unadhani mimi ni mbwa hata unijie kwa fimbo?” Mfilisti huyo akamlaani Daudi kwa miungu yake.

44. Mfilisti akamwambia Daudi, “Njoo kwangu! Mwili wako nitawapa ndege wa angani na wanyama wa porini!”

45. Lakini Daudi akamwambia Goliathi, “Wewe unanijia kwa upanga, mkuki na sime. Lakini mimi ninakujia kwa jina la Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa askari wa Israeli, ambaye wewe umemtukana.

46. Siku ya leo, Mwenyezi-Mungu atakutia mikononi mwangu. Nitakubwaga chini, nitakukata kichwa chako; na miili ya wanajeshi wa Wafilisti nitawapa ndege wa angani na wanyama wa porini. Ndipo dunia nzima itakapojua kuwa Mungu yuko katika Israeli.

47. Watu wote waliokusanyika hapa leo, watajua kuwa Mwenyezi-Mungu hahitaji mikuki wala sime kuwaokoa watu. Hii ni vita ya Mwenyezi-Mungu, naye atawatia nyinyi nyote mikononi mwetu.”

48. Goliathi akaanza tena kumwendea Daudi. Daudi akakimbia mbio kwenda kwenye mstari wa mapambano.

Kusoma sura kamili 1 Samueli 17