Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 17:30-43 Biblia Habari Njema (BHN)

30. Daudi akamgeukia mtu mwingine akamwuliza swali hilohilo; na kila alipouliza, alipata jibu lilelile.

31. Watu fulani ambao walimsikia Daudi alivyosema, walikwenda kumwambia Shauli. Naye Shauli akaagiza aitwe.

32. Daudi akamwambia Shauli, “Mtu yeyote asitishike moyoni mwake kutokana na Mfilisti huyu. Mimi mtumishi wako nitakwenda kupigana naye.”

33. Shauli akamwambia Daudi, “Wewe huwezi kwenda kupigana na Mfilisti yule. Wewe ni kijana tu, lakini mtu huyo amekuwa vitani tangu ujana wake.”

34. Daudi akasema, “Mimi mtumishi wako nimezoea kuchunga kondoo wa baba yangu. Kila wakati simba au dubu akija na kukamata mwanakondoo

35. mimi humfuata na kumshambulia, nikamwokoa mwanakondoo kinywani mwake. Kama simba au dubu akinishambulia, mimi humshika ndevu zake, nikamwangusha na kumuua.

36. Mimi mtumishi wako nimekwisha ua simba wengi na dubu wengi. Sasa, hata yule Mfilisti asiyetahiriwa, ambaye ameyatukana majeshi ya Mungu aliye hai, atakuwa kama hao.

37. Mwenyezi-Mungu ambaye ameniokoa makuchani mwa simba na dubu, ataniokoa kutoka kwa Mfilisti huyu.” Shauli akamwambia, “Nenda; naye Mwenyezi-Mungu awe pamoja nawe.”

38. Shauli akamvisha Daudi mavazi yake ya kivita, akamvika kofia yake ya shaba kichwani na koti lake la kujikinga kifua.

39. Daudi akajifunga upanga wa Shauli, akajaribu kutembea; lakini akashindwa kwa kuwa hakuyazoea mavazi kama hayo. Akamwambia Shauli, “Siwezi kwenda vitani nikiwa nimevaa mavazi haya, kwani mimi sijayazoea.” Kwa hiyo, akayavua.

40. Daudi akachukua fimbo yake mkononi, akajichagulia mawe matano mazuri kutoka kwenye kijito, akayatia katika mfuko wake wa mchungaji. Kombeo lake likiwa tayari mkononi mwake, akaanza kumwendea Goliathi Mfilisti.

41. Yule Mfilisti, naye akaanza kumwendea Daudi, na yule aliyemchukulia ngao yake akiwa mbele yake.

42. Yule Mfilisti alipoangalia na kumwona vizuri Daudi, alimdharau, kwani Daudi alikuwa kijana tu, mwenye afya na wa kupendeza.

43. Goliathi akamwuliza Daudi, “Sasa, hiyo fimbo ni ya nini? Unadhani mimi ni mbwa hata unijie kwa fimbo?” Mfilisti huyo akamlaani Daudi kwa miungu yake.

Kusoma sura kamili 1 Samueli 17