Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 13:5-14 Biblia Habari Njema (BHN)

5. Wafilisti walikuwa na magari 30,000, askari 6,000 wapandafarasi na kikosi cha askari wa miguu wengi kama mchanga wa pwani; wote walipanda juu na kupiga kambi yao huko Mikmashi, mashariki ya Beth-aveni.

6. Waisraeli walipoona wako taabuni (maana walikuwa wanashambuliwa vikali), walianza kujificha. Wengine walijificha mapangoni, wengine mashimoni, wengine kwenye miamba, wengine kwenye makaburi na wengine kwenye visima.

7. Wengine walivuka mto Yordani mpaka katika nchi ya Gadi na nchi ya Gileadi.Lakini Shauli alikuwa bado huko Gilgali na watu wote walimfuata wakitetemeka.

8. Shauli alimngoja Samueli kwa muda wa siku saba, kama Samueli alivyosema. Lakini Samueli hakuja huko Gilgali na watu walianza kumwacha Shauli.

9. Basi, Shauli akawaambia watu, “Nileteeni sadaka yenu ya kuteketezwa na zile za amani.” Naye akatolea sadaka ya kuteketezwa.

10. Mara tu alipokuwa anamaliza kutoa sadaka ya kuteketezwa, Samueli aliwasili. Shauli akatoka nje kwenda kumlaki Samueli na kumsalimia.

11. Samueli akamwuliza, “Umefanya nini?” Shauli akamjibu, “Nilipoona watu wananiacha, na wewe hukuja, katika muda wa siku ulizosema, na tena nilipoona Wafilisti wamejipanga tayari kwa vita huko Mikmashi,

12. nikawaza kwamba Wafilisti watakuja kunishambulia huko Gilgali. Tena nilikuwa bado sijaomba fadhili za Mwenyezi-Mungu. Ndipo nilipolazimika kutolea mimi mwenyewe sadaka ya kuteketezwa.”

13. Samueli akamjibu Shauli, “Umefanya kipumbavu. Hukutii aliyokuamuru Mwenyezi-Mungu, Mungu wako. Kama ungetii, Mwenyezi-Mungu angeudumisha milele ufalme wako juu ya Israeli.

14. Lakini sasa ufalme wako hautadumu kwa kuwa amri aliyokuamuru Mwenyezi-Mungu hukuitii. Mwenyezi-Mungu amejitafutia mtu mwingine ambaye atamtii kwa moyo wote, na huyo ndiye ambaye amemteua kuwa mtawala juu ya watu wake.”

Kusoma sura kamili 1 Samueli 13