Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 13:10-17 Biblia Habari Njema (BHN)

10. Mara tu alipokuwa anamaliza kutoa sadaka ya kuteketezwa, Samueli aliwasili. Shauli akatoka nje kwenda kumlaki Samueli na kumsalimia.

11. Samueli akamwuliza, “Umefanya nini?” Shauli akamjibu, “Nilipoona watu wananiacha, na wewe hukuja, katika muda wa siku ulizosema, na tena nilipoona Wafilisti wamejipanga tayari kwa vita huko Mikmashi,

12. nikawaza kwamba Wafilisti watakuja kunishambulia huko Gilgali. Tena nilikuwa bado sijaomba fadhili za Mwenyezi-Mungu. Ndipo nilipolazimika kutolea mimi mwenyewe sadaka ya kuteketezwa.”

13. Samueli akamjibu Shauli, “Umefanya kipumbavu. Hukutii aliyokuamuru Mwenyezi-Mungu, Mungu wako. Kama ungetii, Mwenyezi-Mungu angeudumisha milele ufalme wako juu ya Israeli.

14. Lakini sasa ufalme wako hautadumu kwa kuwa amri aliyokuamuru Mwenyezi-Mungu hukuitii. Mwenyezi-Mungu amejitafutia mtu mwingine ambaye atamtii kwa moyo wote, na huyo ndiye ambaye amemteua kuwa mtawala juu ya watu wake.”

15. Samueli akaondoka kutoka Gilgali na kwenda huko Gibea katika nchi ya Benyamini.Shauli alipowahesabu watu waliokuwa pamoja naye, aliona wako watu 600 tu.

16. Shauli na Yonathani mwanawe pamoja na watu waliokuwa pamoja nao, walikaa huko Gibea katika nchi ya Benyamini na Wafilisti walipiga kambi huko Mikmashi.

17. Wafilisti walitoka kwenye kambi yao kwenda kuwashambulia wakiwa wako katika vikosi vitatu. Kikosi kimoja kilielekea Ofra katika nchi ya Shuali.

Kusoma sura kamili 1 Samueli 13