Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 12:10-20 Biblia Habari Njema (BHN)

10. Babu zenu wakamlilia Mwenyezi-Mungu, wakisema, ‘Tumefanya dhambi kwa sababu tumekuacha wewe Mwenyezi-Mungu, kwa kutumikia Mabaali na Maashtarothi. Tuokoe kutoka mikononi mwa adui zetu, nasi tutakutumikia’.

11. Ndipo Mwenyezi-Mungu alipomtuma Yerubaali, na baadaye akamtuma Bedani, kisha Yeftha, na mwishowe akanituma mimi Samueli. Kila mmoja wetu aliwaokoa kutoka kwa adui zenu waliowazunguka, nanyi mkaishi kwa amani.

12. Lakini mlipomwona mfalme Nahashi wa Waamoni amekuja kuwashambulia, mkamkataa Mwenyezi-Mungu ambaye ndiye Mfalme wenu, mkaniambia, ‘La! Mfalme ndiye atakayetutawala.’

13. Sasa, mfalme mliyejichagulia ndiye huyu hapa. Mlimwomba Mwenyezi-Mungu awape mfalme, naye amewapa.

14. Kama mkimcha Mwenyezi-Mungu, na kumtumikia, na kusikiliza sauti yake bila kuiasi amri yake, kama nyinyi wenyewe pamoja na mfalme anayewatawala mkimfuata Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, basi mtafanikiwa.

15. Lakini kama hamtasikiliza sauti ya Mwenyezi-Mungu, mkaasi amri yake, basi yeye atapambana nanyi pamoja na mfalme wenu.

16. Kwa hiyo basi, tulieni na kulitazama jambo hilo kubwa ambalo Mwenyezi-Mungu atatenda mbele yenu.

17. Je, sasa si wakati wa kuvuna ngano? Lakini mimi nitamwomba Mwenyezi-Mungu alete radi na mvua, nanyi mtatambua na kuona kuwa uovu wenu mliotenda mbele ya Mwenyezi-Mungu kwa kujitakia mfalme, ni mkubwa.”

18. Basi, Samueli akamwomba Mwenyezi-Mungu, naye akatuma radi na mvua katika siku hiyo. Watu wote wakamwogopa sana Mwenyezi-Mungu na Samueli.

19. Hivyo wakamwambia Samueli, “Tafadhali utuombee sisi watumishi wako kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ili tusife; kwa sababu tumezidisha dhambi zetu kwa uovu huo wa kujitakia mfalme.”

20. Samueli akawajibu, “Msiogope; ingawa mmefanya uovu huu, msiache kumfuata Mwenyezi-Mungu, ila mtumikieni kwa moyo wenu wote.

Kusoma sura kamili 1 Samueli 12