Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 1:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Kulikuwa na mtu mmoja mjini Rama katika nchi ya milima ya Efraimu aitwaye Elkana wa kabila la Efraimu. Yeye alikuwa mwana wa Yerohamu, mwana wa Elihu mwana wa Tohu, mwana wa Sufu.

2. Elkana alikuwa na wake wawili, mmoja aliitwa Hana na wa pili Penina. Penina alikuwa na watoto, lakini Hana hakuwa na watoto.

3. Kila mwaka Elkana alisafiri kutoka Rama kwenda kuabudu na kumtambikia Mwenyezi-Mungu wa majeshi kule Shilo. Huko, watoto wawili wa kiume wa Eli, Hofni na Finehasi, walikuwa makuhani wa Mwenyezi-Mungu.

4. Kila wakati Elkana alipotoa tambiko alimpa mkewe Penina fungu moja la nyama ya tambiko na fungu mojamoja kwa watoto wake wa kiume na wa kike.

5. Lakini Elkana alimpa Hana fungu moja ingawa alikuwa anampenda sana, na Mwenyezi-Mungu hakuwa amemjalia watoto.

6. Lakini Penina, mchokozi wa Hana, daima alikuwa akimkasirisha vikali na kumuudhi Hana kwa kuwa Mwenyezi-Mungu hakumjalia watoto.

7. Mambo haya yaliendelea mwaka baada ya mwaka. Kila mara Hana alipokwenda kwenye nyumba ya Mwenyezi-Mungu, Penina alimkasirisha Hana hata ikawa Hana analia na kukataa kula chochote.

8. Elkana, mumewe, kila mara alimwuliza, “Kwa nini unalia? Kwa nini hutaki kula? Kwa nini una huzuni moyoni mwako? Je, mimi si bora kwako kuliko watoto kumi wa kiume?”

9. Siku moja, walipokuwa wamemaliza kula na kunywa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu huko Shilo, Hana akasimama. Wakati huo, kuhani Eli alikuwa amekaa kwenye kiti karibu na mwimo wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu.

Kusoma sura kamili 1 Samueli 1