Agano la Kale

Agano Jipya

1 Mambo Ya Nyakati 22:2-11 Biblia Habari Njema (BHN)

2. Daudi akatoa amri wageni waliokuwa wanaishi katika nchi ya Israeli wakusanyike, naye akawapangia kazi. Akaweka waashi wachonge vizuri mawe ya kujenga nyumba ya Mungu.

3. Daudi pia akaweka akiba tele ya chuma cha kutengenezea misumari na mafungo ya malango ya nyumba, na akiba tele ya shaba isiyopimika.

4. Mbao za mierezi ambazo Daudi aliletewa na Wasidoni na Watiro zilikuwa hazihesabiki.

5. Daudi akajisemea, “Nyumba ambayo mwanangu Solomoni atamjengea Mwenyezi-Mungu itakuwa ya fahari sana, ya kusifika na tukufu duniani kote. Lakini kwa vile yeye bado angali kijana na bado hana uzoefu mwingi, afadhali nimfanyie matayarisho.” Hivyo basi, Daudi akaweka akiba kubwa sana ya vitu vya ujenzi kabla hajafariki.

6. Ndipo Daudi akamwita Solomoni mwanawe, akamwagiza amjengee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli nyumba.

7. Daudi akamwambia Solomoni, “Mwanangu, nilikusudia moyoni mwangu kumjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu nyumba ili kumtukuza.

8. Lakini Mwenyezi-Mungu aliniambia, ‘Wewe umemwaga damu nyingi kwa kupigana vita vikubwa. Kwa sababu ya damu nyingi ambayo umemwaga mbele yangu hapa duniani, hutanijengea nyumba.

9. Hata hivyo, utapata mwana, ambaye atatawala kwa amani kwa sababu nitampa amani na maadui zake wote wa jirani. Jina lake litakuwa Solomoni, kwa maana katika siku za utawala wake, atailetea Israeli amani na utulivu.

10. Hivyo, yeye ndiye atakayenijengea nyumba. Atakuwa mwanangu nami nitakuwa baba yake, na wazawa wake wataitawala Israeli milele.’

11. Sasa mwanangu, Mwenyezi-Mungu, Mungu wako na awe pamoja nawe ili ufaulu kumjengea nyumba kama alivyosema.

Kusoma sura kamili 1 Mambo Ya Nyakati 22