Agano la Kale

Agano Jipya

1 Mambo Ya Nyakati 21:4-16 Biblia Habari Njema (BHN)

4. Lakini tamko la mfalme lilikuwa na nguvu zaidi dhidi ya Yoabu. Hivyo, Yoabu akaenda katika nchi yote ya Israeli, kisha akarejea Yerusalemu.

5. Yoabu akampelekea mfalme Daudi idadi ya watu: Katika Israeli yote, kulikuwamo wanaume 1,100,000, wenye ujuzi wa kutumia upanga; na katika Yuda kulikuwamo watu 470,000, wenye ujuzi wa kutumia upanga.

6. Lakini Yoabu hakuwahesabu Walawi na Wabenyamini, kwa sababu alichukizwa sana na amri ya mfalme.

7. Mungu hakupendezwa na jambo hilo kwa hiyo akaiadhibu Israeli.

8. Daudi akamwambia Mungu, “Nimetenda dhambi kubwa kwa tendo hili nililolifanya! Lakini nakuomba unisamehe mimi mtumishi wako, kwani nimefanya jambo la kipumbavu kabisa.”

9. Basi, Mwenyezi-Mungu alisema na Gadi, mwonaji wa Daudi, akamwambia,

10. “Nenda umwambie Daudi kwamba mimi Mwenyezi-Mungu ninampa mambo matatu. Ajichagulie mojawapo nami nitamtendea.”

11. Hivyo Gadi akamwendea Daudi na kumwambia, “Mwenyezi-Mungu anasema hivi: Jichagulie mojawapo:

12. Njaa ya miaka mitatu, au miezi mitatu ya maangamizi kutokana na maadui zako ambapo upanga wa maadui zako utakushinda; au siku tatu ambapo Mwenyezi-Mungu atawashambulia kwa upanga wake, awaletee maradhi mabaya nchini, na malaika wake apite kuwaangamiza katika nchi nzima ya Israeli. Sasa amua, ni jibu lipi nitakalompa yeye aliyenituma.”

13. Daudi akamjibu Gadi, “Nimeingia katika mashaka makubwa! Lakini afadhali niadhibiwe na Mwenyezi-Mungu kwani yeye ana huruma sana. Ila nisianguke katika mkono wa mwanadamu.”

14. Basi, Mwenyezi-Mungu akawaletea Waisraeli maradhi mabaya, ambayo yalisababisha vifo vya Waisraeli 70,000.

15. Halafu Mungu akatuma malaika aende kuuharibu Yerusalemu; lakini kabla hajafanya hivyo, Mwenyezi-Mungu akageuza nia yake na kumwambia malaika huyo aliyetekeleza maangamizi, “Basi, yatosha!” Malaika alikuwa amesimama karibu na uwanja wa kupuria nafaka wa Ornani, Myebusi.

16. Daudi akainua macho yake, akamwona huyo malaika wa Mwenyezi-Mungu amesimama kati ya mbingu na dunia, naye ameunyosha upanga wake juu ya Yerusalemu tayari kuuangamiza. Hapo Daudi na wazee wote walikuwa wamevaa mavazi ya gunia, wakaanguka kifudifudi.

Kusoma sura kamili 1 Mambo Ya Nyakati 21