Agano la Kale

Agano Jipya

1 Mambo Ya Nyakati 12:19-37 Biblia Habari Njema (BHN)

19. Askari wengine wa kabila la Manase, walitoroka na kujiunga na Daudi, wakati alipoondoka pamoja na Wafilisti kwenda kupigana na mfalme Shauli. (Lakini hata hivyo, hakuwasaidia maana watawala wa Wafilisti walifanya shauri wamfukuze arudi Siklagi wakisema, “Tutayahatarisha maisha yetu kwa sababu atatutoroka arudi kwa bwana wake Shauli.”)

20. Basi, Daudi alipokuwa Siklagi, watu wafuatao wa kabila la Manase walimwendea: Adna, Yozabadi, Yediaeli, Mikaeli, Yozabadi, Elihu na Silethai. Kila mmoja wao alikuwa kiongozi wa kikosi cha watu 1,000 katika kabila la Manase.

21. Walimsaidia Daudi kupigana na magenge ya washambuliaji, kwani wote walikuwa askari mashujaa na makamanda jeshini.

22. Siku hata siku, watu walijiunga na Daudi kumsaidia, hatimaye akawa na jeshi kubwa sana, kama jeshi la Mungu.

23. Hii ndio idadi ya vikosi vya askari wenye silaha waliojiunga na Daudi huko Hebroni ili kumtwalia ufalme kutoka kwa Shauli, kulingana na neno la Mwenyezi-Mungu:

24. Watu wa kabila la Yuda waliokuwa na mikuki na ngao, walikuwa 6,800. Wote walikuwa na silaha zao.

25. Kutoka kabila la Simeoni, watu 7,100 mashujaa na wenye ujuzi mwingi wa vita.

26. Kutoka kabila la Lawi: Watu 4,600.

27. Yehoyada, wa uzao wa Aroni na wenzake: Watu 3,700.

28. Jamaa ya Sadoki, kijana hodari vitani, yeye pamoja na makamanda ishirini na wawili kutoka ukoo wa baba yake mwenyewe.

29. Kutoka kabila la Benyamini, (kabila la Shauli): Watu 3,000. Wengi wao walibaki waaminifu kwa jamaa ya Shauli;

30. Kutoka kabila la Efraimu: Watu 20,800, watu mashujaa sana tena mashuhuri katika koo zao;

31. Kutoka nusu ya kabila la Manase: Watu 18,000, waliotajwa majina ili waje kumtawaza Daudi awe mfalme.

32. Kutoka kabila la Isakari: Wakuu 200 pamoja na ndugu zao wote waliokuwa chini ya amri yao. Wakuu hao walikuwa na elimu ya kujua mambo ya nyakati na walijua kilichowapasa Waisraeli kufanya.

33. Kutoka kabila la Zebuluni: Watu 50,000; waaminifu na wazoefu wa vita. Walijiandaa na zana za vita za kila namna, lengo lao likiwa ni kumsaidia Daudi tu.

34. Kutoka kabila la Naftali: Makamanda 1,000 pamoja na watu 37,000 wenye ngao na mikuki.

35. Kutoka kabila la Dani: Watu 28,600 wenye silaha tayari kwa vita.

36. Kutoka kabila la Asheri: Watu 40,000 wazoefu wa vita, tayari kwa mapigano.

37. Kutoka kabila la Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase kutoka ngambo ya mto Yordani: Watu 120,000 wenye kila aina ya silaha za vita.

Kusoma sura kamili 1 Mambo Ya Nyakati 12