Agano la Kale

Agano Jipya

Waroma 4:14-25 Biblia Habari Njema (BHN)

14. Maana kama watakaopewa hayo aliyoahidi Mungu ni wale tu wanaoitii sheria, basi, imani haina maana yoyote, nayo ahadi ya Mungu si kitu.

15. Sheria husababisha ghadhabu; lakini kama hakuna sheria, haiwezekani kuivunja.

16. Kwa sababu hiyo, jambo hili lategemea imani, hivyo kwamba ahadi hiyo yatokana na neema ya Mungu, na kwamba ni hakika kuwa ahadi hiyo ni kwa ajili ya wote: Si kwa wale tu wanaoishika sheria, bali pia kwa wale waishio kwa imani kama Abrahamu. Yeye ni baba yetu sisi sote.

17. Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Nimekuweka uwe baba wa mataifa mengi.” Ahadi hiyo ni kweli mbele ya Mungu ambaye Abrahamu alimwamini-Mungu ambaye huwapa wafu uhai, na kwa amri yake, vitu ambavyo havikuwapo huwa.

18. Abrahamu aliamini na kutumaini ingawa hali yenyewe ilikuwa bila matumaini, na hivyo amekuwa baba wa mataifa mengi kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Wazawa wako watakuwa wengi kama nyota!”

19. Alikuwa mzee wa karibu miaka 100, lakini imani yake haikufifia ingawa alijua kwamba mwili wake ulikuwa kama umekufa, na pia mkewe, Sara, alikuwa tasa.

20. Abrahamu hakuionea mashaka ile ahadi ya Mungu; alipata nguvu kutokana na imani, akamtukuza Mungu.

21. Alijua kwamba Mungu anaweza kuyatekeleza yale aliyoahidi.

22. Ndiyo maana Mungu alimkubali kuwa mwadilifu.

23. Inaposemwa, “Alimkubali,” haisemwi kwa ajili yake mwenyewe tu.

24. Jambo hili linatuhusu sisi pia ambao tunamwamini Mungu aliyemfufua Yesu, Bwana wetu, kutoka kwa wafu.

25. Yeye alitolewa auawe kwa ajili ya dhambi zetu, akafufuka ili tufanywe waadilifu.

Kusoma sura kamili Waroma 4