Agano la Kale

Agano Jipya

Mathayo 27:6-24 Biblia Habari Njema (BHN)

6. Makuhani wakuu wakazichukua zile fedha, wakasema, “Haifai kuziweka katika hazina ya hekalu kwa maana ni fedha za damu.”

7. Basi, wakashauriana, wakazitumia kununua shamba la mfinyanzi liwe mahali pa kuzika wageni.

8. Ndio maana mpaka leo shamba hilo linaitwa Shamba la Damu.

9. Hivyo maneno ya nabii Yeremia yakatimia: “Walichukua vipande thelathini vya fedha, thamani ya yule ambaye watu wa Israeli walimtia bei,

10. wakanunua nazo shamba la mfinyanzi, kama Bwana alivyoniagiza.”

11. Yesu alisimamishwa mbele ya mkuu wa mkoa. Basi, mkuu wa mkoa akamwuliza, “Je, wewe ndiwe Mfalme wa Wayahudi?” Yesu akamwambia, “Wewe umesema.”

12. Lakini makuhani wakuu na wazee walipokuwa wanamshtaki, hakujibu neno.

13. Hivyo Pilato akamwuliza, “Je, husikii mashtaka hayo yote wanayotoa juu yako?”

14. Lakini Yesu hakumjibu hata neno moja; hata huyo mkuu wa mkoa akashangaa sana.

15. Ilikuwa kawaida wakati wa sikukuu ya Pasaka mkuu wa mkoa kuwafungulia Wayahudi mfungwa mmoja waliyemtaka.

16. Wakati huo kulikuwa na mfungwa aliyejulikana sana, jina lake Baraba.

17. Hivyo, watu walipokusanyika pamoja, Pilato akawauliza, “Mwataka nimfungue yupi kati ya wawili hawa, Baraba ama Yesu aitwaye Kristo?”

18. Alisema hivyo maana alijua wazi kwamba walimleta kwake kwa sababu ya wivu.

19. Pilato alipokuwa amekaa katika kiti cha hukumu, mke wake akampelekea ujumbe: “Usijitie katika shauri la mtu huyu mwema, maana leo nimeteseka sana katika ndoto kwa sababu yake.”

20. Lakini makuhani wakuu na wazee wakawashawishi watu waombe Baraba afunguliwe na Yesu auawe.

21. Mkuu wa mkoa akawauliza, “Ni yupi kati ya hawa wawili mnayetaka nimfungue?” Wakamjibu, “Baraba!”

22. Pilato akawauliza, “Sasa, nifanye nini na Yesu aitwaye Kristo?” Wote wakasema, “Asulubiwe!”

23. Pilato akauliza, “Kwa nini? Amefanya ubaya gani?” Wao wakazidi kupaza sauti: “Asulubiwe!”

24. Basi, Pilato alipotambua kwamba hafanikiwi chochote na kwamba maasi yalikuwa yanaanza, alichukua maji, akanawa mikono mbele ya ule umati wa watu, akasema, “Mimi sina lawama juu ya kifo cha mtu huyu; shauri lenu wenyewe.”

Kusoma sura kamili Mathayo 27