Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 8:21-35 Biblia Habari Njema (BHN)

21. Huna sehemu yoyote wala haki katika kazi hiyo kwa maana moyo wako hauko sawa mbele ya macho ya Mungu.

22. Kwa hiyo, tubu ubaya wako huu na umwombe Bwana naye anaweza kukusamehe fikira kama hizo.

23. Ni dhahiri kwangu kwamba umejaa wivu mkali na u mfungwa wa dhambi!”

24. Simoni akajibu, “Tafadhali, niombeeni kwa Bwana lisije likanipata lolote kati ya hayo mliyosema.”

25. Baada ya Petro na Yohane kutoa ushuhuda wao na kuutangaza ujumbe wa Bwana, walirudi Yerusalemu. Walipokuwa wanarudi walihubiri Habari Njema katika vijiji vingi vya Samaria.

26. Malaika wa Bwana alimwambia Filipo, “Jitayarishe uende kusini kupitia njia inayotoka Yerusalemu kwenda Gaza.” (Njia hiyo hupita jangwani).

27. Basi, Filipo akajiweka tayari, akaanza safari. Wakati huohuo kulikuwa na Mwethiopia mmoja, towashi, ambaye alikuwa anasafiri kuelekea nyumbani. Huyo mtu alikuwa mkurugenzi maarufu wa hazina ya Kandake, malkia wa Ethiopia. Alikuwa amekwenda huko Yerusalemu kuabudu na wakati huo alikuwa anarudi akiwa amepanda gari la kukokotwa.

28. Alipokuwa anasafiri, alikuwa akijisomea kitabu cha nabii Isaya.

29. Basi, Roho Mtakatifu akamwambia Filipo, “Nenda karibu na gari hilo ukafuatane nalo.”

30. Filipo akakimbilia karibu na gari, akamsikia huyo mtu akisoma katika kitabu cha nabii Isaya. Hapo Filipo akamwuliza, “Je, unaelewa hayo unayosoma?”

31. Huyo mtu akamjibu, “Ninawezaje kuelewa bila mtu kuniongoza?” Hapo akamwalika Filipo apande juu, aketi pamoja naye.

32. Basi, sehemu ya Maandiko Matakatifu aliyokuwa anasoma ilikuwa hii:“Alikuwa kama kondoo anayepelekwa kuchinjwa;kimya kama vile mwanakondoo anapokatwa manyoya,yeye hakutoa sauti hata kidogo.

33. Alifedheheshwa na kunyimwa haki.Hakuna atakayeweza kuongea juu ya kizazi chake,kwa maana maisha yake yameondolewa duniani.”

34. Huyo Mwethiopia akamwambia Filipo, “Niambie, huyu nabii anasema juu ya nini? Anasema mambo haya juu yake yeye mwenyewe au juu ya mtu mwingine?”

35. Basi, Filipo akianzia na sehemu hiyo ya Maandiko Matakatifu, akamweleza Habari Njema juu ya Yesu.

Kusoma sura kamili Matendo 8