Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 28:4-15 Biblia Habari Njema (BHN)

4. Wenyeji wa pale walipokiona kile kiumbe kinaninginia kwenye mkono wake waliambiana, “Bila shaka mtu huyu amekwisha ua mtu, na ingawa ameokoka kuangamia baharini, ‘Haki’ haitamwacha aendelee kuishi!”

5. Lakini Paulo alikikungutia kile kiumbe motoni na hakuumizwa hata kidogo.

6. Wale watu walikuwa wakitazamia kwamba angevimba au angeanguka chini na kufa ghafla. Baada ya kungojea kwa muda mrefu bila kuona kwamba Paulo amepatwa na jambo lolote lisilo la kawaida, walibadilisha fikira zao juu yake, wakasema kuwa yeye ni mungu.

7. Karibu na mahali pale palikuwa na mashamba ya Publio, mkuu wa kile kisiwa. Publio alitukaribisha kirafiki, tukawa wageni wake kwa siku tatu.

8. Basi, ikawa kwamba baba yake Publio alikuwa amelala kitandani, mgonjwa wa homa na kuhara. Paulo alikwenda kumwona na baada ya kusali, akaweka mikono yake juu ya mgonjwa, akamponya.

9. Kutokana na tukio hilo, wagonjwa wote katika kile kisiwa walikuja wakaponywa.

10. Watu walitupatia zawadi mbalimbali na wakati tulipoanza tena safari, walitia ndani ya meli masurufu tuliyohitaji.

11. Baada ya miezi mitatu tulianza tena safari yetu kwa meli moja ya Aleksandria iitwayo “Miungu Pacha”. Meli hiyo ilikuwa imetia nanga kisiwani wakati wote wa baridi.

12. Tulifika katika mji wa Sirakusa, tukakaa hapo kwa siku tatu.

13. Toka huko tulingoa nanga, tukazunguka na kufika Regio. Baada ya siku moja, upepo ulianza kuvuma kutoka kusini, na baada ya siku mbili tulifika bandari ya Potioli.

14. Huko tuliwakuta ndugu kadhaa ambao walituomba tukae nao kwa juma moja. Hivi ndivyo tulivyopata kufika Roma.

15. Ndugu wa kule Roma walipopata habari zetu, wakaja kutulaki kwenye soko la Apio na Mikahawa Mitatu. Paulo alipowaona alimshukuru Mungu, akapata moyo.

Kusoma sura kamili Matendo 28