Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 25:4-19 Biblia Habari Njema (BHN)

4. Lakini Festo alijibu, “Paulo atabaki kizuizini kule Kaisarea na mimi nitakwenda huko karibuni.

5. Waacheni viongozi wenu waende huko pamoja nami wakatoe mashtaka yao juu yake kama amefanya chochote kiovu.”

6. Festo alikaa nao kwa muda wa siku nane au kumi hivi, kisha akarudi Kaisarea. Kesho yake alikwenda barazani, akaamuru Paulo aletwe ndani.

7. Wakati Paulo alipofika, Wayahudi waliokuwa wametoka Yerusalemu walimzunguka wakaanza kutoa mashtaka mengi mazitomazito ambayo hawakuweza kuthibitisha.

8. Kwa kujitetea, Paulo alisema, “Mimi sikufanya kosa lolote kuhusu sheria ya Wayahudi, wala kuhusu hekalu, wala kumhusu Kaisari.”

9. Festo alitaka kujipendekeza kwa Wayahudi na hivyo akamwuliza Paulo, “Je, ungependa kwenda Yerusalemu na huko ukahukumiwe mbele yangu kuhusu mashtaka haya?”

10. Paulo akajibu, “Nasimama mbele ya mahakama ya Kaisari, na papa hapa ndipo ninapopaswa kupewa hukumu. Kama unavyojua vizuri, sikuwatendea Wayahudi ubaya wowote.

11. Basi, ikiwa nimepatikana na kosa linalostahili adhabu ya kifo, siombi kusamehewa adhabu hiyo. Lakini kama hakuna ukweli katika mashtaka waliyotoa watu hawa, hakuna awezaye kunikabidhi kwao. Nakata rufani kwa Kaisari!”

12. Basi, baada ya Festo kuzungumza na washauri wake, akamwambia Paulo, “Umekata rufani kwa Kaisari, basi, utakwenda kwa Kaisari.”

13. Siku chache baadaye, mfalme Agripa na Bernike walifika Kaisarea ili kutoa heshima zao kwa Festo.

14. Walikuwa huko siku kadhaa naye Festo akamweleza mfalme kesi ya Paulo: “Kuna mtu mmoja hapa ambaye Felisi alimwacha kizuizini.

15. Nilipokwenda Yerusalemu makuhani wakuu na wazee wa Wayahudi walimshtaki na kuniomba nimhukumu.

16. Lakini mimi niliwajibu kwamba si desturi ya Waroma kumtoa mtu aadhibiwe kabla mshtakiwa hajakutana na washtaki wake ana kwa ana na kupewa fursa ya kujitetea kuhusu hayo mashtaka.

17. Basi, walipofika hapa sikukawia, ila nilifanya kikao mahakamani kesho yake, nikaamuru mtu huyo aletwe.

18. Washtaki wake walisimama lakini hawakutoa mashtaka maovu kama nilivyokuwa ninatazamia.

19. Ila tu walikuwa na mabishano kadhaa pamoja naye kuhusu dini yao na kuhusu mtu mmoja aitwaye Yesu ambaye alikufa, lakini Paulo anashikilia kwamba yu hai.

Kusoma sura kamili Matendo 25