Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 17:9-17 Biblia Habari Njema (BHN)

9. Wakawafanya Yasoni na wenzake watoe dhamana, kisha wakawaacha waende zao.

10. Usiku, wale ndugu waliwahimiza Paulo na Sila waende Berea. Mara tu walipofika huko, walikwenda katika sunagogi la Wayahudi.

11. Watu wa huko walikuwa wasikivu zaidi kuliko wale wa Thesalonike. Waliupokea ule ujumbe kwa hamu kubwa, wakawa wanayachunguza Maandiko Matakatifu kila siku, ili kuona kama yale waliyosema Paulo na Sila yalikuwa kweli.

12. Wengi wao waliamini na pia wanawake wa Kigiriki wa tabaka la juu na wanaume pia.

13. Lakini, Wayahudi wa Thesalonike walipogundua kwamba Paulo alikuwa anahubiri neno la Mungu huko Berea, walikwenda huko, wakaanza kufanya fujo na kuchochea makundi ya watu.

14. Wale ndugu wakamsindikiza haraka aende pwani lakini Sila na Timotheo walibaki Berea.

15. Wale ndugu waliomsindikiza Paulo walikwenda pamoja naye mpaka Athene. Kisha, wakarudi pamoja na maagizo kutoka kwa Paulo kwamba Sila na Timotheo wamfuate upesi iwezekanavyo.

16. Paulo alipokuwa anawasubiri Sila na Timotheo huko Athene, moyo wake ulighadhibika sana alipoona jinsi mji huo ulivyokuwa umejaa sanamu za miungu.

17. Alijadiliana na Wayahudi na watu wengine waliomcha Mungu katika sunagogi; na kila siku alikuwa na majadiliano mahali pa hadhara pamoja na wote wale waliojitokeza.

Kusoma sura kamili Matendo 17