Agano la Kale

Agano Jipya

Marko 2:3-16 Biblia Habari Njema (BHN)

3. wakati mtu mmoja aliyepooza alipoletwa kwake akiwa amechukuliwa na watu wanne.

4. Kwa sababu ya huo umati wa watu, hawakuweza kumpeleka karibu na Yesu. Basi, wakatoboa sehemu ya paa iliyokuwa juu ya mahali alipokuwa Yesu. Walipokwisha pata nafasi, wakamteremsha huyo mtu akiwa amelala juu ya mkeka.

5. Yesu alipoona imani yao, akamwambia huyo mtu aliyepooza, “Mwanangu, umesamehewa dhambi zako.”

6. Baadhi ya waalimu wa sheria waliokuwa wameketi hapo wakawaza mioyoni mwao,

7. “Anathubutuje kusema hivyo? Anamkufuru Mungu! Hakuna mtu awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake.”

8. Yesu alitambua mara mawazo yao, akawaambia, “Mbona mnawaza hivyo mioyoni mwenu?

9. Ni lipi lililo rahisi zaidi: Kumwambia mtu huyu aliyepooza, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kumwambia, ‘Inuka! Chukua mkeka wako utembee?’

10. Basi, nataka mjue kwamba Mwana wa Mtu anayo mamlaka ya kuwasamehe watu dhambi duniani.” Hapo akamwambia huyo mtu aliyepooza,

11. “Nakuambia simama; chukua mkeka wako uende nyumbani!”

12. Mara, watu wote wakiwa wanamtazama, huyo mtu akainuka, akauchukua mkeka wake, akaenda zake. Watu wote wakashangaa na kumtukuza Mungu wakisema, “Hatujapata kamwe kuona jambo kama hili.”

13. Yesu alikwenda tena kando ya ziwa. Umati wa watu ukamwendea, naye akaanza kuwafundisha.

14. Alipokuwa akipita, akamwona Lawi mwana wa Alfayo, ameketi katika ofisi ya ushuru. Yesu akamwambia, “Nifuate!” Lawi akasimama, akamfuata.

15. Baadaye, Yesu alikuwa amekaa mezani, nyumbani kwa Lawi, kula chakula. Watozaushuru wengi na wenye dhambi walikuwa wamemfuata Yesu na wengi wao wakawa wamekaa mezani pamoja naye na wanafunzi wake.

16. Basi, baadhi ya waalimu wa sheria ambao walikuwa Mafarisayo walipomwona Yesu akila pamoja na watu wenye dhambi na watozaushuru, wakawauliza wanafunzi wake, “Kwa nini anakula pamoja na watozaushuru na wenye dhambi?”

Kusoma sura kamili Marko 2