Sura

  1. 1
  2. 2
  3. 3
  4. 4
  5. 5
  6. 6
  7. 7
  8. 8
  9. 9
  10. 10
  11. 11
  12. 12
  13. 13
  14. 14
  15. 15
  16. 16

Agano la Kale

Agano Jipya

Marko 15 Biblia Habari Njema (BHN)

Yesu anapelekwa kwa Pilato

1. Kulipopambazuka, makuhani wakuu walifanya shauri pamoja na wazee, waalimu wa sheria na Baraza lote, wakamfunga Yesu pingu, wakampeleka na kumkabidhi kwa Pilato.

2. Pilato akamwuliza Yesu, “Je, wewe ni Mfalme wa Wayahudi?” Yesu akajibu, “Wewe umesema.”

3. Makuhani wakuu wakamshtaki Yesu mambo mengi.

4. Pilato akamwuliza tena Yesu, “Je, hujibu neno? Tazama wanavyotoa mashtaka mengi juu yako.”

5. Lakini Yesu hakujibu neno, hata Pilato akashangaa.

Yesu anahukumiwa kufa

6. Kila wakati wa sikukuu ya Pasaka, Pilato alikuwa na desturi ya kuwafungulia mfungwa mmoja waliyemtaka.

7. Basi, kulikuwa na mtu mmoja aitwaye Baraba, ambaye alikuwa amefungwa pamoja na waasi wengine kwa kusababisha uasi na mauaji.

8. Watu wengi wakamwendea Pilato wakamwomba awafanyie kama kawaida yake.

9. Pilato akawauliza, “Je, mwataka niwafungulieni Mfalme wa Wayahudi?”

10. Alisema hivyo kwa sababu alijua wazi kwamba makuhani wakuu walimkabidhi Yesu kwake kwa sababu ya wivu.

11. Lakini makuhani wakuu wakawachochea watu wamwombe Pilato awafungulie Baraba.

12. Pilato akawauliza tena, “Basi, sasa mwataka nifanye nini na mtu huyu mnayemwita Mfalme wa Wayahudi?”

13. Watu wote wakapaza sauti tena: “Msulubishe!”

14. Lakini Pilato akawauliza, “Kwa nini! Amefanya ubaya gani?” Lakini wao wakazidi kupaza sauti, “Msulubishe!”

15. Pilato alitaka kuuridhisha huo umati wa watu; basi, akamwachilia Baraba kutoka gerezani. Akaamuru Yesu apigwe viboko, kisha akamtoa asulubiwe.

Askari wanamdhihaki Yesu

16. Kisha askari walimpeleka Yesu ndani ukumbini, katika ikulu, wakakusanya kikosi kizima cha askari.

17. Wakamvika vazi la rangi ya zambarau, wakasokota taji ya miiba, wakamwekea kichwani.

18. Wakaanza kumsalimu, “Shikamoo Mfalme wa Wayahudi!”

19. Wakampiga kichwani kwa mwanzi, wakamtemea mate; wakampigia magoti na kumsujudia.

20. Baada ya kumdhihaki, walimvua lile joho, wakamvika nguo zake, kisha wakampeleka kumsulubisha.

Yesu anasulubiwa

21. Walipokuwa njiani, walikutana na mtu mmoja aitwaye Simoni, mwenyeji wa Kurene. Yeye alikuwa baba yao Aleksanda na Rufo, na wakati huo alikuwa akitoka shambani. Basi, wakamlazimisha achukue msalaba wa Yesu.

22. Kisha wakampeleka Yesu mpaka mahali palipoitwa Golgotha, maana yake, mahali pa Fuvu la Kichwa.

23. Wakampa divai iliyochanganywa na manemane, lakini yeye alikataa kunywa.

24. Basi, wakamsulubisha, wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura waamue nani angepata nini.

25. Ilikuwa saa tatu asubuhi walipomsulubisha.

26. Na shtaka dhidi yake lilikuwa limeandikwa, “Mfalme wa Wayahudi.”

27. Pamoja naye waliwasulubisha wanyanganyi wawili, mmoja upande wake wa kulia na mwingine upande wake wa kushoto. [

28. Hapo yakatimia Maandiko Matakatifu yanayosema, “Aliwekwa kundi moja na waovu.”]

29. Watu waliokuwa wanapita mahali hapo walimtukana, wakitikisa vichwa vyao na kusema, “Aha! Wewe mwenye kuvunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu!

30. Sasa, shuka msalabani ujiokoe mwenyewe!”

31. Nao makuhani wakuu pamoja na waalimu wa sheria walimdhihaki wakisema, “Aliwaokoa wengine, lakini kujiokoa mwenyewe hawezi!

32. Ati yeye ni Kristo, Mfalme wa Israeli! Basi, na ashuke kutoka msalabani ili tuone na kuamini.” Hata watu wale waliosulubiwa pamoja naye walimtukana.

Yesu anakufa msalabani

33. Tangu saa sita mchana mpaka saa tisa giza likaikumba nchi yote.

34. Saa tisa alasiri Yesu akalia kwa sauti kubwa, akasema, “Eloi, Eloi, lema sabakthani?” Maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”

35. Baadhi ya watu waliosimama pale waliposikia hivyo, walisema, “Sikiliza! Anamwita Elia.”

36. Mtu mmoja akakimbia, akaichovya sifongo katika siki, akaiweka juu ya mwanzi, akampa anywe akisema, “Hebu tuone kama Elia atakuja kumteremsha msalabani!”

37. Yesu akapaza sauti kubwa, akakata roho.

38. Basi, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu mpaka chini.

39. Jemadari mmoja aliyekuwa amesimama mbele yake alipoona kwamba Yesu alikata roho namna hiyo, akasema, “Kweli mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu!”

40. Walikuwako pia wanawake waliotazama kwa mbali, miongoni mwao akiwa Maria Magdalene, Salome, na Maria mama wa kina Yakobo mdogo na Yose.

41. Hawa walimfuata Yesu alipokuwa Galilaya na kumtumikia. Kulikuwa na wanawake wengine wengi waliokuja Yerusalemu pamoja naye.

Yesu anazikwa

42. Wakati wa jioni ulikuwa umekwisha fika. Hiyo ilikuwa siku ya Maandalio, yaani siku inayotangulia Sabato.

43. Hapo akaja Yosefu mwenyeji wa Arimathaya, mjumbe wa Baraza Kuu, aliyeheshimika sana. Yeye pia alikuwa anatazamia kuja kwa ufalme wa Mungu. Basi, alimwendea Pilato bila woga, akaomba apewe mwili wa Yesu.

44. Pilato alishangaa kusikia kwamba Yesu alikuwa amekwisha kufa. Basi, akamwita jemadari, akamwuliza kama Yesu alikuwa amekufa kitambo.

45. Pilato alipoarifiwa na huyo jemadari kwamba Yesu alikuwa amekwisha kufa, akamruhusu Yosefu kuuchukua mwili wake.

46. Hapo Yosefu akanunua sanda ya kitani, akauteremsha chini huo mwili, akauzungushia sanda. Akauweka katika kaburi lililokuwa limechongwa mwambani, kisha akavingirisha jiwe kubwa mbele ya mlango.

47. Nao Maria Magdalene na Maria mama yake Yose walipaona hapo alipolazwa.