Agano la Kale

Agano Jipya

Marko 13:8-20 Biblia Habari Njema (BHN)

8. Taifa moja litapigana na taifa lingine; ufalme mmoja utapigana na ufalme mwingine; kila mahali kutakuwa na mitetemeko ya ardhi na njaa. Mambo haya ni kama tu maumivu ya kwanza ya kujifungua mtoto.

9. “Lakini nyinyi jihadharini. Maana watu watawapelekeni mahakamani, na kuwapigeni katika masunagogi. Mtapelekwa mbele ya watawala na wafalme kwa sababu yangu, ili mpate kunishuhudia kwao.

10. Lakini lazima kwanza Habari Njema ihubiriwe kwa mataifa yote.

11. Nao watakapowatieni nguvuni na kuwapeleka mahakamani, msiwe na wasiwasi juu ya yale mtakayosema; saa ile itakapofika, semeni chochote mtakachopewa, maana si nyinyi mtakaosema, bali Roho Mtakatifu.

12. Ndugu atamsaliti ndugu yake auawe; baba atamsaliti mwanawe; watoto nao watawashambulia wazazi wao na kuwaua.

13. Watu wote watawachukieni nyinyi kwa sababu ya jina langu. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokolewa.

14. “Mtakapoona ‘Chukizo Haribifu limesimama mahali ambapo si pake, (msomaji na atambue maana yake), hapo, walioko Yudea wakimbilie milimani.

15. Aliye juu ya paa la nyumba asishuke kuingia nyumbani mwake kuchukua kitu.

16. Aliye shambani asirudi nyuma kuchukua vazi lake.

17. Ole wao kina mama waja wazito na wanaonyonyesha siku hizo!

18. Ombeni ili mambo hayo yasitukie nyakati za baridi.

19. Maana wakati huo kutakuwa na dhiki ambayo haijatokea tangu Mungu alipoumba ulimwengu mpaka leo, wala haitatokea tena.

20. Kama Bwana asingepunguza siku hizo hakuna binadamu ambaye angeokolewa. Lakini kwa ajili ya wateule wake, Bwana amezipunguza siku hizo.

Kusoma sura kamili Marko 13