Agano la Kale

Agano Jipya

Marko 12:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Yesu alianza kusema nao kwa mifano: “Mtu mmoja alilima shamba la mizabibu. Akalizungushia ukuta, na katikati yake akachimba kisima cha kusindikia divai, akajenga mnara pia. Akalikodisha shamba hilo kwa wakulima, akasafiri hadi nchi ya mbali.

2. Wakati wa mavuno, alimtuma mtumishi wake kwa wale wakulima, akamletee sehemu ya mazao ya shamba lake.

3. Wale wakulima wakamkamata, wakampiga, wakamrudisha mikono mitupu.

4. Akamtuma tena mtumishi mwingine; huyu pia wakamwumiza kichwa na kumtendea vibaya.

5. Yule mwenye shamba akatuma mtumishi mwingine tena ambaye hao wakulima walimuua. Wengine wengi waliotumwa, baadhi yao walipigwa, na wengi wakauawa.

6. Alibakiwa bado na mtu mmoja, yaani mwanawe mpenzi. Mwishowe akamtuma huyo akisema, ‘Watamjali mwanangu.’

7. Lakini hao wakulima wakaambiana, ‘Huyu ndiye mrithi, basi, tumuue ili urithi wake uwe wetu!’

8. Kwa hiyo wakamkamata, wakamuua na kumtupa nje ya lile shamba la mizabibu.

9. “Basi, mwenye shamba atafanya nini? Atakuja kuwaangamiza hao wakulima na kulikodisha hilo shamba la mizabibu kwa watu wengine.

10. Je, hamjasoma Maandiko haya?‘Jiwe walilokataa waashisasa limekuwa jiwe kuu la msingi.

11. Bwana ndiye aliyefanya jambo hili,nalo ni la ajabu sana kwetu.’”

12. Makuhani wakuu, waalimu wa sheria na wazee walifahamu ya kwamba mfano huo ulikuwa unawahusu. Kwa hiyo walijaribu kumtia nguvuni, lakini waliogopa umati wa watu. Basi, wakamwacha, wakaenda zao.

13. Basi, baadhi ya Mafarisayo na wafuasi wa kikundi cha Herode walitumwa ili wamtege Yesu kwa maneno yake.

Kusoma sura kamili Marko 12